RC MACHA AKABIDHI GARI JIPYA KWA RUWASA MKOA WA SHINYANGA
Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amemkabidhi gari jipya STN 2943 kwa Mhandisi Julieth Payovela ambaye ni Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga, katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga huku akisisitiza kuwa ikatumike kwa kadiri ya lengo kusudiwa la serikali.
Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 28 Oktoba, 2024 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude, pamoja na watumishi mbalimbali kutoka RUWASA na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambapo amemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha watumishi kutekeleza kazi zao kwa ufanisi zaidi na kuwahudumia wananchi kwa wakati na kuwafikia kwa haraka zaidi.
"Kwanza tumshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwawezesha watumishi katika Wizara, Sekta na Ofisi zake zote ili kurahisisha utekelezaji na usimamizi wa shughuli za kila siku kama ambavyo imefanyika kwa wenzetu hawa RUWASA Mkoa wa Shinyanga, niwaombe kwenda kutumia gari hili kwa kadiri ya lengo lililokusudiwa na Serikali na wala isiwe vinginevyo," amesema RC Macha.
Kando na hayo, ameitaka RUWASA Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha kuwa gari hili linatunzwa kwa maslahi mapana ya Serikali ili lidumu muda mrefu na lifanyiwe matengenezo stahiki pale inapohitajika kufanya hivyo huku akiwataarifu waalikwa wa hafla hii kuwa anatambua, anathamini na kuheshimu zaidi kazi, ubunifu, weledi na utendaji kazi wa Meneja RUWASA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth.
Kwa upande wake Mhandisi Julieth amemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha ofisi yake kupata kitendea kazi ambacho kinakwenda kuongeza ufanisi na uboreshaji wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku, huku akimpongeza RC Macha kwa kuendelea kuisaidia RUWASA katika utekelezaji wa kazi za kila siku mkoani Shinyanga.
Upokeaji wa gari hili jipya STN 2943 kwa RUWASA unakwenda kurahisisha usimamizi na uboreshaji wa miradi inayotekelezwa, aidha utoaji wa huduma ya maji Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Maji inaendelea kununua vitendea kazi kwa watendaji vikiwemo pikipiki, Magari n.k.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464