JUMLA ya vijana 61,wakike wakiwa 3 na wakiume 58 wamehitimu mafunzo ya jeshi la akiba maarufu kama mgambo ambao waliweka kambi katika Kata ya Shagihilu Wilaya ya Kishapu tangu Juni 10, 2024.
Akizungumza katika sherehe ya kufunga mafunzo hayo , Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Dkt, Joseph Mkude amewataka vijana hao kuwa waadilifu na wazalendo kwa nchi yao pamoja na kuyatumia mafunzo waliyoyapata kwa maslahi yao na nchi nzima kwa ujumla.
“Tunatumaini kwamba mtatusaidia vyema katika kupunguza uhalifu. Tunategemea kwamba mtaungana na wenzenu ambao walishapata mafunzo na kwa kusaidiana na majeshi mengine ili kusaidia Wilaya ya Kishapu kubaki salama, amani na utulivu. Kwa mafunzo mliopewa tunaamini kwamba sasa Kishapu inaenda kuwa na utulivu.” Amesema Dkt, Mkude.
Aidha kutokana sababu ya baadhi ya vijana kushindwa kumaliza mafunzo hayo kutokana na sababu mbalimbali Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa jamii kuwaandikisha watoto wao kushiriki katika mafunzo ili watoto wao wasijekukosa fursa mbalimbali hapo baadae.
Kwa upande wake Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Kishapu Meja Linus Elias amesema kuwa wahitimu hao wamehitimu mafunzo kwa kiwango kinachotakiwa na watakuwa tayari muda wote kulitumikia taifa lao.
Katika risala yao wahitimu wa mafunzo ya jeshi la akiba wamesema wamejengewa kikakamavu katika kujilinda wao wenyewe, raia na mali zao ikiwa ni pamoja na mafunzo ya matumizi ya silaha, ujanja wa porini, usomaji wa ramani, sheria za mgambo, kwata mbalimbali, elimu ya uraia, kuzuia na kupambana na rushwa, zima moto na mafunzo ya ujasiriamali.
Aidha wamesema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza uhalifu katika jamii kwa kudhibiti wizi wa mazao, uvunjaji wa maduka na kupambana na magendo
Pia Dkt, Mkude alitumia furusa hii kuwakumbusha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kujiandikisha kwenye Daftari la Mkazi litakalo anza Tarehe 11-20 Oktoba 2024 kwaajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464