Header Ads Widget

CCM NA SERIKALI WILAYANI KWIMBA WAPONGEZA JUHUDI ZA KASHWASA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI NGUDU

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Serikali Wilayani Kwimba, Mkoani Mwanza, wameeleza kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na KASHWASA katika kutatua tatizo la ukosefu wa maji safi na salama katika Mji wa Ngudu.

Tukio hilo lilijitokeza leo, tarehe 2 Oktoba 2024, wakati Mkurugenzi Mtendaji wa KASHWASA, Eng. Patrick Nzamba, alipofika katika Ofisi za CCM na kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, kwa lengo la kuelezea mikakati iliyowekwa katika utatuzi wa changamoto hiyo.

Eng. Nzamba alizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, akieleza kuwa tayari Mkandarasi amepatikana kwa ajili ya kubadilisha mabomba yasiyokidhi viwango, kazi ambayo itaanza mara baada ya malipo ya awali kutolewa. Aliongeza kuwa KASHWASA kwa kushirikiana na MWAUWASA, wapo katika hatua za mwisho za kufufua visima viwili vya zamani ili kuongeza uzalishaji wa maji katika mji huo.

Akitoa kauli ya serikali, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija, alithibitisha kuwa ofisi yake imeridhishwa na hatua zinazochukuliwa na KASHWASA. Alipongeza juhudi hizo na kusisitiza umuhimu wa kutoa taarifa za haraka kuhusu hali ya huduma ya maji kwa wananchi.

Ziara hiyo ilihudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Eng. Ramadhan Mramba, ambaye alishiriki katika majadiliano hayo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya mji wa Ngudu.

Post a Comment

0 Comments