Header Ads Widget

IDADI YA WATOTO WENYE UTAPIAMLO MANISPAA YA KINONDONI YAPUNGUA

 


Na Patricia Kimelemeta

MANISPAA ya Kinondoni imeendelea kutoa elimu ya lishe kwa wananchi hali iliyosaidia kupungua kwa idadi ya watoto wanaokutwa na utapiamlo.

Awali, katika taarifa iliyotolewa kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM),kilichofanyika Novemba 2023, ilionyesha kuwa   mwezi Oktoba  peke yake, watoto 150 wenye umri kuanzia miezi miwili hadi miaka minane wamekutwa na utapiamlo  uliokithiri hali iliyosababisha baadhi yao kupewa rufaa na kupelekwa  kwenye vituo vinavyotoa huduma ya lishe vilivyopo kwenye manispaa hiyo.

Programu hiyo ilizinduliwa Desemba Mwaka 2021 ambayo itatekelezwa hadi Mwaka 2026 ambapo kila Mkoa na Halmashauri zake  wametakiwa kushirikiana na Asasi za kiraia ili kutekeleza afua tano za elimu, afya, lishe,malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama.

Akizungumza hivi karibuni, Ofisa Lishe Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanamvua Zuberi amesema kuwa, ripoti ya miezi miwili iliyopita ambayo ni Julai na Agosti  imeonyesha kuwa, Kuna idadi ndogo ya watoto wenye udumavu ikilinganishw na kipindi kilichopita.

Amesema kuwa katika kipindi hicho jumla ya watoto 196 walikutwa na utapiamlo kutokana na ukosefu wa lishe bora ambao ni sawa na asilimia 1.2 ambao ni kati ya watoto 16902 waliopimwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Amesema kuwa, watoto hao waligundulika baada ya kufanyiwa vipimo kwenye kliniki mbalimbali zilizopo kwenye Manispaa  hiyo hali iliyosababisha baadhi yao kukutwa na utapiamlo na kupelekwa kwenye vituo vya matibabu.

Amesema kuwa, wale waliobainika wa afadhari kidogo  walipewa tiba na kuruhuswa kurudi nyumbani na wale waliobainika wameathiriwa zaidi walipelekwa hospitali ya Mwananyamala na vituo vingine vya kutibia watoto wenye utapiamlo ili waweze kupatiwa matibabu.

 " Wakati tunatekeleza Programu ya PJT-MMMAM,  tulibaini zaidi ya  watoto 150 ndani ya mwezi mmoja walikua na utapiamlo,huku baadhi yao wakiwa na utapiamlo uliokithiri, hali hiyo ilitulazimu  kuwapa rufaa kwa kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma ya matibabu waweze kuwa na uangalizi maalum wa afya zao lakini pia wazazi na walezi wao walikua wakipewa elimu ya lishe.

" Lakini sasa hivi hali ya utapiamlo inaendelea kupungua siku hadi siku ambapo mwezi Julai na Agosti tumepata watoto 196 Waliogundulika kuwa na utapiamlo,' amesema Mwanamvua.

Ameongeza kuwa, toka Serikali itekeleze Programu ya  PJT-MMMAM kumekua na mwamko mkubwaa wa utoaji wa elimu yya Lishe kwa jamii ambayo inashirkisha wadau mbalimbali wakiwamo wananchi wenyewe, jambo ambalo limechangia kuwepo kwa mafanikio.

Amesema kuwa, hata hivyo, Manispaa hiyo imekua ikiwapima watoto  hali ya lishe mara kwa mara kwa wale  wanaofikishwa kliniki ili wazazi na walezi wao waweze kuzingatia ulaji unaofaa kwa watoto wao, jambo ambalo limekua likizaa matunda.

Amesema kuwa, elimu hiyo imekua ikitolewa kwa kushirikiana  na watalaam wa afya ambalo wamekuwa wakiwaelimisha  wazazi na walezi wao   namna ambavyo wanapaswa kuwapikia watoto wao na kuwapa lishe bora jambo ambalo linaweza kukuza ubongo wao na kuwapa uchangamfu.

Amesema kuwa, licha ya kutoa elimu hiyo, lakini baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa hawazingatii ulaji unaofaa kwa watoto, jambo ambalo limesababisha  kupata utapiamlo, hivyo basi wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali Ili kuhakikisha elimu ya Malezi, makuzi na maendeleo ya awali inawafikia wananchi wengi zaidi kuanzia ngazi ya mtaa Hadi Wilaya Ili waweze kubadili mtindo wa ulaji.

Amesema kuwa, Manispaa hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa, wanatokomeza utapiamlo kwa Wananchi  ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya chakula bora kinachofaa kwa ajili ya kuimarisha afya  ya mtoto ya mwili na akili, jambo ambalo litasaidia kukua katika Hali ya utimilifu.

Amesema kuwa, wataendelea kuwahimiza wazazi kuwapeleka watoto kliniki ili waweze kupimwa na kujua hali yao ya ukuaji ya watoto, Ili wale watakaobainika wana matatizo wawaishwe kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi," amesema.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya Kaya Foundation, Anapili Ngome amesema kuwa,  baadhi ya wazazi wannashindea kutekeleza afua za lishe jambo ambalo limechangia kuendelea kujitokeza kwa udumavu katika baadhi ya maeneo.

" Tangu tuanze kutekeleza proramu ya PJT-MMMAM elimu ya lishe imekua ilitolewa kuanzia ngazi ya mtaa, jambo ambalo limesaidia kupunguza udumavu japo baadhi ya wananchi wanashindwa kutekeleza afua za lishe kwa makusudi.

Asasi za kiraia tumekua mstari wa mbele kushirikiana na serikali ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wengi zaidi, "amesema  Ngome.

Baadhi ya wananchi wamewema kuwa, serikali imeweza kuwaweka maofisa lishe kuanzia ngazi ya mtaa ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wengi zaidi, jambo ambalo linawexa kupunguza idadi ya watoto wenye utapiamlo.

" Kumekua na mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na serikali kuanzisha utaratibu wa kuwaweka maofisa lishe ngazi ya kata ili waweze kupata mitaani kitoa elimu ya lishe, jambo ambalo linachangia kuongezeka wa uelewa wananchi kwa namna gani wanapaswa kuwapa vyakula vyenye virutubisho watoto wao,"amesema Joseph Yunus.

Programu jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM)  inalenga kuongeza kasi ya mafanikio yanayopatikana katika huduma kwa kuboresha ushirikiano wa kisekta katika utoaji wa huduma za Malezi jumuishi kwa watoto na kuongeza uratibu wa huduma na kuimarisha utekelezaji wa Sheria na sera zinazohusu masuala hayo ikiwa ni pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, sera ya afya ya mwaka 2007, sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 2008, sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambazo zimelenga kushughulikia mahitaji yote ya mtoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane.


Mwisho



Post a Comment

0 Comments