Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imewataka viongozi
wa vyama vya siasa kurejea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya
9, kipengele "H", kinachozielekeza mamlaka za nchi na taasisi zake
kuzingatia juhudi za kutokomeza rushwa. Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa
Shinyanga, Mwamba Masanja, ameonya kuhusu tabia ya wagombea wa nafasi
mbalimbali za uongozi wanaojihusisha na utoaji rushwa ili waweze kuchaguliwa.
Na Mwandishi wetu kutoka Shinyanga.
Maelekezo
haya yametolewa na Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga, Mwamba
Masanja, wakati akizungumza na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani
Shinyanga, katika muendelezo wa semina elekezi ya TAKUKURU kwa makundi
mbalimbali.
Kuhusu baadhi ya viongozi kuwahadaa wananchi kwa rushwa wakati wa uchaguzi, baadhi ya viongozi wa CCM wilayani humo wamesema imefika wakati sasa viongozi kuanza kupambana na rushwa ndani ya vyama vyao kabla ya kutoka nje kwa wananchi kwakuwa picha halisi iliyopo ni tofauti na matarajio ya watanzania walio wemgi ambapo katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga vijijini Mch. Emmanuel Lukanda amesema viongozi wanapaswa kuwa na hofu ya mungu kwa kuikataa rushwa wazi wazi na sio vinginevyo.
Afisa wa TAKUKURU upande wa elimu kwa jamii Mohamed Doo ameielezea rushwa kuwa ni kosa la jinai na kuainisha kuwa adhabu yake ni kifungo, au faini au adhabu zote mbili kwa pamoja yaani kifungo na faini ambapo amewataka viongozi wa vyama vya siasa kujiepusha na makoso yote yanayohusiana na rushwa.