JOWUTA yataka sheria za kazi kuwalinda wafanyakazi katika vyombo vya habari.
.UTPC yaomba serikali kuingilia kati.
Mwandishi wetu,Singida
Chama cha Wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini(JOWUTA) kimetaka serikali kusimamia sheria za kazi kwa wafanyakazi katika vyombo vya habari kama zilivyo sekta nyingine ili waandishi wapate haki na stahiki zao.
Mwenyekiti wa Taifa wa JOWUTA,Mussa Juma ametoa wito huo jana wakati akizungumza katika mkutano mkuu wa Umoja wa klabu za waandishi wa habari Tanzania(UTPC)mkoani Singida.
Juma alisema, waandishi wa habari wengi nchini, wamekuwa wakipitia madhila makubwa ikiwepo kutoajiwa ,kutokuwa na mikataba wala kuwa na bima za afya na Maisha.
"Sekta nyingine tunaona hatua zinachukuliwa kama mwajiri halipi mishahara wafanyakazi ama mwajiri anakaa na mtumishi zaidi ya mwaka bila kumpa hata mikataba"amesema.
Amesema JOWUTA imejitahidi mara kadhaa kufikisha hoja za maslahi bora ya waandishi serikali lakini bado hatua hazichukuliwi za kutosha.
"Kikubwa waandishi tusiwe wanyonge,tusione taaluma hii ni watu wenye shida ,tujitokeze kutetea maslahi yetu bila hofu kwanì taaluma hii haina tofauti na taaluma nyingine katika kupata katika kazi na haki za kisheria"amesema.
Juma amesema, zaidi ya asilimia 80 ya waandishi nchini hawa mikataba ya ajira wala bima jambo ambalo linapunguza ari na uhuru wa utendaji kazi wao .
Akizungumza katika mkutano huo,Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC,Kenneth Simbaya aliomba serikali kulifanyia kazi suala la maslahi kwa waandishi wa habari.
Simbaya alimuomba aliyekuwa Mgeni rasmi katika mkutano.huo,Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Adolf Mkenda kufikisha hoja za changamoto za waandishi katika baraza la mawaziri.
"Kama alivyosema awali Mwenyekiti wa JOWUTA sekta ya habari kuna changamoto nyingi tunaomba mnapokutana viongozi mlizumgumze na hili jambo la maslahi ya waandishi wetu"alisema
Hata hivyo, Juma aliomba wanahabari nchini kuendelea kujiunga na JOWUTA ili kuwa na sauti ya pamoja kudai haki na stahiki zao.
Akizungumza katika mkutano huo,Profesa Mkenda aliahidi wizara yake kushirikiana na wanahabari nchini kwani anatambua umuhimu wa vyombo vya habari.
Alisema anazijua changamoto za wanahabari ikiwepo pia suala la kitaaluma na akaahidi kushirikiana na wadau kuboresha mitaala katika vyuo vya uandisbi wa habari.
Waziri Profesa Mkenda pia alizungumzia mabadiliko makubwa ya sekta ya elimu nchini ambayo yanalenga kuboresha sekta hiyo na kutoa wahitimu wenye ujuzi na uwezo kujiajiri na kuajiriwa.
Awali Rais wa UTPC ,Deogratius Nsokolo alitoa taarifa ya ya maendeleo ya utendaji ya UTPC na mikakati ijayo ya maboresho makubwa ya UTPC.
Katika mkutano huo, wanachama wa UTPC walipitisha taarifa ya mwaka,taarifa ya fedha na mikakati ijayo ya UTPC.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464