SHUWASA YATIA SAINI MKATABA WA BILIONI 9 WA KUIJENGEA UWEZO TAASISI

SHUWASA YATIA SAINI MKATABA WA BILIONI 9 WA KUIJENGEA UWEZO TAASISI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

KAMPUNI ya GOPAInfra ya nchini Ujerumani,ikishirikiana na Kampuni ya Superlit Consulting Ltd ya Tanzania,wamesaini Mkataba na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), wa kuijengea uwezo mamlaka hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake ya uboreshaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi.
Mkataba huo umesainiwa leo Novemba 4,2024 katika Ofisi za SHUWASA.

Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya GOPAInfra Stefan Doerner, akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, amesema Mkataba huo wa kuijengea uwezo SHUWASA, utatekelezwa ndani ya miaka minne,kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi wa Shinyanga.
Naye Mkurugezi wa Kampuni ya Superlit Consulting LTD Mhandisi Fortunatus Kasimbi, ambao watafanya kazi na Kampuni hiyo ya GOPAInfra katika kuijengea uwezo SHUWASA, amesema Mkataba huo utaimarisha shughuli za Mamlaka hiyo na kufanyika kwa usahihi na ubora unaotakiwa kwa kuangalia mapungufu yaliyopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA Mhandisi Yusup Katopola akizungumza kwenye hafla hiyo ya utiaji saini, amesema Mkataba huo ni sehemu mojawapo ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga, ambao unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye thamani ya Euro Milioni 76.
Aidha, Juni 6 2022 Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), zilitia Saini Mkataba wa Ufadhili wa mkopo wa riba nafuu wa Euro Milioni 76 (Takribani Shilingi Bilioni 200), kwaajili ya mradi mkubwa wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga ambao unahusisha kuijengea uwezo taasisi, ujenzi wa mtandao wa majisafi kilomita 287; ukarabati wa mtandao chakavu wa majisafi kilomita 100 na ujenzi wa matangi mawili (Kolandoto-lita 1,500,000 na Didia- lita 250,000).

“Mkataba huu utatekelezwa ndani ya miaka minne, kuanzia leo terehe 4.11.2024 na utakwenda hadi  Novemba 2028, na utakuwa msaada mkubwa sana kwetu sisi SHUWASA, na kutoa huduma bora kwa wananchi”amesema Mhandisi Katopola.

Amesema pia katika utekelezaji wa Mkataba huo, watafanya kazi kwa ushirikiano na Kampuni hizo, kwa kuhakikisha malengo ya Serikali ya uboreshaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwenye maeneo ambayo yanahudumiwa na SHUWASA, ambayo ni Manispaa ya Shinyanga,Tinde na Iselamagazi, kwamba yanakuwa na huduma bora.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola (kushoto)akisaini Mkataba wa kujiengea uwezo Taasisi hiyo, (kulia)ni Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya GOPAInfra ya Ujerumani Stefan Doerner.
Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya GOPAInfra ya Ujerumani Stefan Doerner (kulia)akisaini Mkataba wa kuijengea uwezo SHUWASA, (kushoto) ni Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola (kushoto)akiwa na Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya GOPAInfra Stefan Doerner (kulia)wakionyesha Mkataba ambao wamesaini wa kuijengea uwezo SHUWASA.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola (kushoto)akiwa na Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya GOPAInfra Stefan Doerner (kulia)wakikabidhiana Mkataba.
Hafla ya utiaji saini Mkataba ikiendelea.
Hafla ya utiaji saini Mkataba ikiendelea.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464