RC MACHA AKEMEA UPOTOSHAJI WALENGWA TASAF KUFANYA KAZI AJIRA ZA MUDA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amewasihi waandishi wa habari kuandika habari kwa usahihi juu ya mpango wa kunuru Kaya Maskini TASAF, na kuondoa upotoshaji ambao huenezwa na baadhi ya watu kuhusu walengwa kufanya kazi za ajira za muda mfupi.
Amebainisha hayo leo Novemba 7,2024 wakati akifungua mafunzo ya TASAF kwa waandishi wa habari mkoani Shinyanga, ambayo yaliombwa na Klabu ya Waandishi wa habari mkoani huo SPC.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha juu ya Walengwa wa TASAF kufanya kazi za ajira za muda mfupi,pamoja na kuwapiga picha na kuandika maneneo ya upotoshaji, kuwa Walengwa hao wanafanyishwa kazi kama wafungwa,jambo ambalo amelipinga kuwa siyo sahihi.
Amesema kutokana na waandishi wa habari kupata mafunzo hayo ya TASAF, ni vyema sasa wakaandika habari kwa usahihi na kuielimisha jamii, pamoja na kuondoa upotoshaji juu ya Walengwa wa TASAF kufanya kazi za ajira za muda, kuwa wasiwafananishe na wafungwa na kutafsiri kufanya kazi ni adhabu.
“Kuna jambo moja la upotoshaji ambalo nawaomba waandishi wa habari mkaelimishe umma kuhusu ajira za muda, ni kwamba Walengwa kufanya kazi siyo tatizo, bali wanafanya kazi kama watu wengine na siyo adhabu, hata Wafungwa kufanya kazi siyo adhabu pia, adhabu yao wao ni kutengwa na kuishi kwa kuamuliwa kila kitu,”amesema Macha.
Aidha, amesema Walengwa wa TASAF kufanya kazi ni sehemu ya kujiongeza kipato na kuondokana na umaskini, na baadae kuja kuondolewa kwenye mpango huo sababu watakuwa wameimalika kiuchumi.
“Dhumuni la Serikali kuanzisha mpango huu wa TASAF ni kuimarisha ustawi wa maisha ya Watanzania wote, na Rais Samia Suluhu Hassan, anapenda kuona watu wote wanakuwa na maisha mazuri na kupata mahitaji ya msingi ya mwanadamu, kama vile chakula,mavazi,makazi,elimu,maji na afya,”amesema Macha.
Amewataka pia Walengwa wa TASAF ambao wameimalika kiuchumi na kuondolewa kwenye mpango huo, waache tabia ya kulalamika kwanini wameondolewa na hata kukimbilia kwenye vyombo vya habari, kwamba kutoendelea kusaidiwa ni heshima kubwa, huku akisisitiza pia kwenye uingizwaji wa walengwa wapya, zoezi hilo liwe shirikishi ili wapatikane watu sahihi ambao ni maskini.
Katika hatua nyingine Macha amewataka waandishi wa habari, kwamba waandike habari pia za kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao utafanyika novemba 27 mwaka huu,ili wachague viongozi watakaowaletea maendeleo.
Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano kutoka TASAF Makao Makuu Japhet Boaz,akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray,amesema mpango wa TASAF wa kunusuru Kaya maskini ulianza mwaka 2013 baada ya kuzinduliwa mwezi Agost 2012, ukilenga kuhudumia Kaya milioni 1.2 ambazo zilikuwa zinaishi chini ya mstari wa umaskini wa chakula.
“Matokeo ya utafiti wa mapato na matumizi ya Kaya binafsi kwa Tanzania Bara ya mwaka 2011/2012, ulifanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),taarifa ya utafiti huo ilionyesha asilimia 9.7 ya Watanzania walikuwa wanaishi chini ya mstari wa umaskini wa chakula,”amesema Boaz.
Aidha,amesema kipindi cha pili cha mpango kilizinduliwa mwezi Februari 2020 na kimeendelea kuhudumia zaidi ya Kaya milioni 1.37, na utekelezaji wake unafanyika kwenye halmashauri 184 Tanzania bara pamoja na Ugunja na Pemba kwa Zanzibar.
Amesema kwa kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi juni 2024 mpango umehawilisha ruzuku ya jumla ya Sh.milioni 945.5 kwa Kaya milioni 1.3 zilizoandikishwa kwenye mpango,huku Kaya zipatazo 534,606 zimelipwa kwa njia ya kielektroniki.
Amesema katika mpango wa kutoa ajira za muda kwa Kaya za walengwa, kwamba jumla ya miradi 27,863 iliibuliwa na wananchi na kutekelezwa na walengwa wa mpango, na kiasi cha sh.bilioni 117.3 kimetumika kulipa ujira kwa Kaya za walengwa 662,374 kwa kushiriki katika kutekeleza miradi hiyo, na kutengeneza miundombinu yenye faida kwa jamii nzima kama miradi ya umwagiliaji,upandaji miti,mabwawa,utunzaji wa ardhi na barabara zinazounganisha vijiji,na mitaa.
Amesema kutokana na shughuli za kuongeza kipato ili kukuza uchumi kwa walengwa, kwamba hadi kufikia Juni 2024 jumla ya Kaya 394,500 zenye wastani wa watu milioni 1.8, zilikuwa zimejikomboa kutoka kwenye umaskini uliokithiri na hivyo kutoka katika mpango wa TASAF.
Amesema katika kuendelea kukuza uchumi wa Kaya za walengwa,kwamba vimeundwa vikundi vya kuweka akiba na kukopesha, na kwamba hadi kufikia juni 2024 kulikuwa na jumla ya vikundi 60,342, vyenye wanachama 838,241, na vikundi hivyo vimekusanya Sh. bilioni 7.9, na kukopeshana Sh.bilioni 3.2 kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kuwaongezea kipato.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye mafunzo ya TASAF kwa waandishi wa habari.
Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano kutoka TASAF Makao Makuu Japhet Boaz akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mratibu wa TASAF Mkoa wa Shinyanga Dotto Maligisa akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo ya TASAF yakiendelea kwa waandishi wa habari.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464