RC MACHA AWASIHI WAKULIMA WA PAMBA KUNG'OA MAOTEA SHAMBANI,KABLA YA KUCHUKULIWA HATUA


RC MACHA AWASIHI WAKULIMA WA PAMBA KUNG'OA MAOTEA SHAMBANI,KABLA YA KUCHUKULIWA HATUA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amewasihi Wakulima wa Pamba kung'oa maotea shambani kabla ya kuchukuliwa hatua.
Amesema suala la kung'oa maotea shambani ni lazima kisheria,sababu maotea hayo yanazalisha wadudu,na ni hatari kwa samba la mtu mwingine kushambuliwa na wadudu hao ambaye tayari ameshasafisha shamba lake kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo cha pamba 2024/2025.

Amebainisha hayo leo Novemba 10,2024, kwenye kikao cha Maofisa ugani na Watendaji wa Kata zote wilayani Kishapu, akiwa ameambatana na Balozi wa Pamba nchini Aggrey Mwanri.
Amesema muda wa ung'oaji wamaotea shambani umeshapita,lakini wakulima wengi bado hawajayang'oa,na hivyo kutoa muda wa siku mbili kwamba kuanzia tarehe 11-12 Novemba mwaka huu,kwamba wale Wakulima ambao bado hawajang'oa maotea watachukuliwa hatua.

"Wakulima ambao bado hawajang'oa maotea shambani wachukuliwe hatua,kung'oa maotea ni lazima sababu ni hatari kwa shamba la mtu mwingine kumpelekea wadudu,"amesema Macha.
Aidha,amewataka Maofisa ugani wakafanye kazi ya kusaidia wakulima wa Pamba, kutoa elimu ya kilimo chenye tija, na kwamba kipimo cha utendaji wao kazi katika msimu wa mwaka huu wa kilimo cha pamba, ni wakulima kuvuna kilo 800 kwa hekali moja na kutoka kilo 100,200 na 300.

Amesema serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,tayari yenyewe imeshajipanga kurejesha heshima ya zao la pamba, ambapo Maofisa ugani wameshapewa pikipiki,vishikwambi,vifaa vya kupimia udongo,sare,kuleta mbegu za pamba zenye ubora, pamoja na matrekta 24 ambayo yatapunguza gharama za kilimo kwa wakulima.
"Mheshimiwa Rais Samia aliponiapisha alinipa maagizo ya kurudisha heshima ya zao la Pamba mkoani Shinyanga,kazi ndiyo nimeanza katika msimu huu wa 2024/2025 nataka wakulima walime kilimo chenye tija na kupata mavuno mengi na kuinuka kiuchumi, na taifa kwa ujumla kupata mapato,"amesema Macha.

Balozi wa Pamba nchini Aggrey Mwanri, amesema septemba 15 ndiyo ulikuwa mwisho wa kung'oa maotea shambani, na novemba 15, itakuwa siku ya kuanza kupanda zao la Pamba Shambani,lakini wakulima wengi wilayani Kishapu bado hawajang'oa maotea.
"Nakupongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,kwa kutekeleza maagizo ya Rais Samia ya kurejesha heshima ya Pamba,jitihada zako nimeziona,Rais Samia wakati wa hotuba yake ya kwanza alitaja zao la pamba kwamba ifikapo 2025 zizalishwe tani Milioni 1,zao hili ndiyo mkombozi mkubwa wa Wakulima," amesema Mwanri.

Aidha,amewataka pia Wakulima wa Pamba,kwamba wanapolima zao hilo wasichanganye na mazao mengine, pamoja na kufuata kanuni bora za unyunyiziaji wadudu,uvunaji,huku akisisitiza kutoichafua pamba hiyo kwa kuweka mchanga,mawe na mafuta ya kenge.
Nao Maofisa ugani wa Halmashuri ya wilaya ya Kishapu,wameahidi kutekeleza maagizo yote ambayo yametolewa na viongozi.

Katika kikao hicho liliambatana pia na zoezi la utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya upuliziaji wa dawa kua wadudu kwenye zao la pamba, pamoja na uzinduzi wa awamu ya pili la ung'oaji na uchomaji wa maotea shambani.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu William Jijimya akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akizungumza kwenye kikao hicho.
Balozi wa Pamba nchini Aggrey Mwanri akizungumza kwenye kikao hicho.
Balozi wa Pamba nchini Aggrey Mwanri akitoa elimu ya unyunyiziaji dawa ya kuuwa wadudu katika zao la Pamba kwa Maofisa Ugani ili wakaelimishe Wakulima.
Uzinduzi wa uchomaji wa maotea shambani awamu ya pili ukiendelea.
Picha ya pamoja ikipigwa pamoja na Maofisa Ugani.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464