DC MTATIRO AZINDUA BODI YA AFYA NA KAMATI YA USIMAMIZI HOSPITALI YA HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA
MKUU wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro amezindua Rasmi Bodi ya Afya, na Kamati ya usimamizi katika Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,huku akizitaka kutoingilia majukumu ya watalaamu.
Uzinduzi huo umefanyika leo novemba 21,2024 katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, na kabla ya hapo ulifanyika kwanza uchaguzi wa viongozi wa bodi na kamati.
Mtatiro akizungumza kwenye uzinduzi huo,amewataka viongozi na wajumbe wa bodi na kamati, kwamba wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao, wasijeingilia masuala ya kitaalamu, bali waulize kwanza taratibu zikoje, ili wazungumze lugha moja na kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
“Viongozi wa bodi,kamati, na wajumbe, nendeni mkazisome vizuri hizo nyaraka ili mjue majukumu yenu, na mfanye kazi vizuri ya uboreshaji wa huduma za afya,pamoja na kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya,”amesema Mtatiro.
Amesisitiza pia katika vikao vyao visiwe vya kutanguliza posho, bali wawe wanaenda na masuala ya kujadili changamoto ambazo bado zinaikabili huduma ya afya na kuzitafutia ufumbuzi, ili kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi.
Aidha,amesema serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetoa fedha nyingi kuboresha sekta ya afya, ambapo miundombinu ya afya imeimalika,ikiwamo na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa pamoja na madawa,huku akimpongeza Rais kwa kasi yake kubwa ya utekelezaji wa maendeleo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje,amewapongeza viongozi waliochaguliwa kusimamia Hospitali ya Halmashauri hiyo, na kuwasihi kusimamia ubora wa utoaji huduma za afya kwa wananchi.
Awali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Nuru Yunge, akisoma taarifa amesema halmashauri hiyo ina Hospitali Moja, Vituo vya Afya Vitano, na Zahanati 44, na ina wakazi 468,611 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Ametaja majukumu ya Bodi ya Afya,ambayo pia yanarandana na Kamati ya usimamizi kwa kiasi kikubwa,kuwa ni kuhakikisha jamii inapata huduma bora za afya,upatikanaji wa Rasilimali na mgawanyo wake kwa kuzingatia mahitaji ya ngazi zote,kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato,itashirikiana na kamati za afya za vituo,sekta binafsi, na wadau wengine, kwa nia ya kuinua kiwango cha afya na utoaji wa huduma.
Majukumu mengine ni kuratibu na kusimamia shughuli za maendeleo ya afya, ukiwamo mpango wa maendeleo afya msingi (MMAM)katika eneo la Mamlaka husika,kuhakikisha kuwepo kwa wafanyakazi kulingana na ikama ya halmashauri, pamoja na kuwajibika kufanya shughuli za ufuatiliaji na tathimini za utoaji huduma za afya.
Amesema bodi pia itawajibika kwa jamii katika kusimamia utoaji wa huduma bora za afya,upatikanaji wa dawa na vitendea kazi muhimu, pamoja na kuhakikisha kuna kuwepo na mahusiano mazuri kati ya watoa huduma na watumiaji.
Amesema kwa upande wa kamati za usimamizi,ni kuhakikisha jamii inashirikishwa katika kutambua matatizo,kuweka kipaumbele,kupanga,kuchagia huduma,kufuatilia na kutathimini utoaji wa huduma za afya,pia kuhakikisha jamii inakuwa na uwezo wa kusimamia huduma za afya,pamoja na kushughulikia malalamiko ya watumiaji huduma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Hospitali hiyo ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Adrian Joseph, ameomba ushirikiano ili kufanikisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi, huku akiwasihi wajumbe wa bodi, kwamba wafanye kazi vizuri na wataalamu.
Aidha,Kamati ya Bodi ya Afya ya Hospitali ya Halmanshauri ya wilaya ya Shinyanga, inaongozwa na Mwenyekiti Adrian Joseph na Makamu wake ni Peter Kasoga, huku Kamati ya usimamizi wa Hospitali hiyo Mwenyekiti wake ni Samson Dotto Ipililo, na Kamati hiyo itakaa madarakani kwa muda wa miaka mitatu.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Afya na Kamati ya Usimamizi katika Hospitali ya Halmshauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Afya na Kamati ya Usimamizi katika Hospitali ya Halmshauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Afya na Kamati ya Usimamizi katika Hospitali ya Halmshauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Afya na Kamati ya Usimamizi katika Hospitali ya Halmshauri ya wilaya ya Shinyanga
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Afya na Kamati ya Usimamizi katika Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mwenyekiti wa Bodi ya Afya Hospitali ya wilaya ya Shinyanga Adrian Joseph akizungumza.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk,Nuru Yunge akisoma majukumu ya Bodi ya Afya na Kamati ya Usimamizi.
Viongozi wakiwa meza kuu kwenye uzinduzi wa Bodi ya Afya ya Hospitali ya wilaya ya Shinyanga na Kamati ya Usimamizi.
Wajumbe wa Bodi ya Afya na Kamati ya Usimamizi katika Hospitali ya wilaya ya Shinyanga.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464