CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Shinyanga, kimelalamikia ongezeko la vituo vya kupigia kura katika Manispaa ya Shinyanga,huku wakidai kuchelewa kushirikishwa juu ya ongezeko la vituo hivyo.
Hayo yamebainishwa leo novemba 26,2024, na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema kwa taarifa za awali waliambiwa kwamba Manispaa ya Shinyanga itakuwa na vituo 163 vya kupigia kura,kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini ghafla vikaongezwa vituo 122 bila ya wao kupewa taarifa mapema ili watafute Mawakala.
"Chadema tumeanza kuhofia kutengenezewa ushindi wa bao la mkono kwenye huu uchaguzi wa serikali za mitaa,kumeanza kuandaliwa kuwepo kwa vituo hewa vya kupigia kura,"amesema Ntobi
"Sisi awali tuliambiwa kutakuwa na vituo 163 vya kupigia kura, jana jioni ndiyo tukapewa taarifa kuwa kuna ongezeko la vituo vingine, kwamba tutafute Mawakala, huku zoezi la kuapisha Mawakala likiwa tayari limeshapita ambapo ni Novemba 23 na 24," ameongeza Ntobi
Aidha, amesema licha ya kupambana kutafuta Mawakala, na kuelezwa wataapishwa,lakini cha ajabu wasimamizi wasaidizi ngazi ya Kata, amedai kwamba wamegoma kuapisha Mawakala wao, kwa kisingizio wanakikao na Mkurugenzi.
Kesho novemba 27, ni siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa,kwa wananchi kupiga kura na kuchagua Wenyeviti wa Vijiji,Vitongoji, Mitaa pamoja na wajumbena leo ndiyo mwisho wa kufunga kampeni za kudani wagombea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464