WALENGWA TASAF WAONDOKANA NA UMASKINI WAJENGA NYUMBA ZA KISASA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
WALENGA wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini TASAF katika Manispaa ya Shinyanga,wameelezea mafanikio ambayo wameyapata kupitia mpango huo,kwa kuondokana na umaskini huku wakijenga nyumba za kisasa.
nyumba ya awali ya Mlengwa wa TASAF Anna Shija Makonda.
Wamebainisha hayo leo novemba 8,2024 wakati waandishi wa habari wakiwa na Maofisa wa TASAF, walipotembea Kaya zao ilikuona mafanikio ambayo wameyapata kupitia mpango huo na kisha kuondokana na umaskini.
Mmoja wa wanufaika hao wa TASAF Anna Shija Makonda, kutoka Kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga, amesema yeye aliingia kwenye mpango wa TASAF mwaka 2015, na alikuwa na maisha magumu huku akila Mlo mmoja kwa siku na watoto wake Saba,pamoja na kuishi kwenye nyumba ya tope.
nyumba ya sasa.
Amesema wakati akiendelea kupokea Ruzuku ya TASAF Sh.56,000, alijiunga pia kwenye kikundi cha akiba na kukopeshana, na baada ya kuvunja kikoba alipata Sh. Laki 8, fedha ambayo alinunua Nguruwe watatu, ambapo aliwazalisha hadi wakafika 8, na baadae aliwauza baadhi na kuanza ujenzi wa nyumba ya kisasa.
Ameendelea kusimulia kuwa sasa hivi hali yake ya maisha ni nzuri siyo maskini tena, na ameshatoka kwenye mpango huo ili kuzipatia nafasi Kaya zingine ambazo ni maskini ili na zenyewe zinufaike na mpango huo na kuinuka kiuchumi.
“naishukuru sana serikali kwa kuanzia mpango huu wa TASAF mimi sasa hivi siyo maskini tena, naishi kwenye nyumba ya kisasa, nasomesha watoto wangu hadi wajukuu, nina miliki mifugo nguruwe 8, bata watano na kuku 10,”amesema Anna.
Mlengwa mwingine Mushi Kumi, anasema yeye ameshaondoka kwenye mpango wa TASAF,baada ya kuimarika kiuchumi,na sasa wamejiunga kwenye kikundi cha akina na kukopeshana, na wapo wanachama 7 na kila wiki huchangisha sh.2,000 ili kikundi hicho kiendelee kuwainua kiuchumi zaidi kupitia biashara zao.
Aidha, kwa nyakati tofauti Walengwa hao wametoa wito kwa wenzao ambao bado wapo kwenye mpango huo, kuwa fedha hizo za Ruzuku ambazo wanapewa, wazitumie vizuri kwa malengo kusudiwa na siyo kuzifanyia Anasa ili wainuke kiuchumi.
Naye Afisa ufuatiliaji Mpango wa TASAF Shinyanga, Tabu Maro, amewataja Walengwa wa TASAF ambao wameondolewa kwenye Mpango huo baada ya kuimarika kiuchumi, kwamba katika Manispaa ya Shinyanga wapo 1,500 na waliobaki ni 2,600,Wilayani Shinyanga waliondolewa 2,500 waliobaki 8,200.
Walengwa TASAF ambao hawapo tena kwenye mpango huo mara baada ya kuimarika kiuchumi na sasa wana kikundi chao cha akiba na kukopesha.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464