WAZIRI WA UJENZI INNOCENT BASHUNGWA AFANYA ZIARA USHETU KUKAGUA NA KUKABIDHI KAZI ZA DHARURA KWA WAKANDARASI UJENZI MADARAJA
Na Marco Maduhu,USHETU
WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa,amefanya ziara Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga,kukagua na kukabidhi kazi za dharura kwa Wakandarasi ujenzi wa madaraja, pamoja na kuzungumza na wananchi wa Bugomba kwenye mkutano wa hadhara.
ziara hiyo imefanyika leo Novemba 30,2024 ambapo Waziri huyo alikuwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali,akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.
Bashungwa amesema, Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mfuko kurudisha barabara na madaraja korofi, ambayo yaliharibiwa na mvua za Elinino na Kimbunga Hidaya, kwamba kwa nchi nzima ametoa kiasi cha fedha Sh.bilioni 868 ili kukarabati miundombinu hiyo.
Amesema kwa upande wa Ushetu Rais Samia, ametoa kiasi cha fedha Sh.bilioni 18.5 ili kukarabati Madaraja Manne ambayo yaliharibiwa na mvua, likiwamo ambalo linaunganisha Halmashauri ya Ushetu na Geita.
"Halmashauri hii ya Ushetu kuna madaraja matatu ambayo yanatekelezwa yenye thamani ya sh.bilioni 13.5, ambayo baadhi tumeyakagua leo, lakini kuna daraja jingine ambalo linajengwa la kuunganisha Ushetu na Geita,hivyo kwenye ardhi hii ya Ushetu kutakuwa na madaraja manne yanayotekelezwa yenye thamani ya sh.bilioni 18.5," amesema Bashungwa.
Aidha,amemuagiza Meneja Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samweli Mwambungu, kwamba awasimamie vyema Wakandarasi ili watekeleze kazi hizo kwa mujibu wa Mkataba,pamoja na thamani ya fedha kuonekana kwa kujengwa kwa ubora unaotakiwa.
Amemsihi pia kuhakikisha anapeleka Mkandarasi kwenye ujenzi wa daraja ambalo linaunganisha Mkoa wa Geita ili aanze kazi mara moja,na kwamba ndani ya Mwaka Mmoja madaraja hayo yote yanatakiwa yawe yameshakamilika kujengwa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amempongeza Rais Samia kwa kutoa fedha ili kujengwa Madaraja hayo, na kwamba wananchi walikuwa wakipata shida na madaraja hayo ambayo yamekuwa mkombozi kwao, na ikizingatiwa Halmashauri ya Ushetu wengi wao ni Wakulima wa Tumbaku.
Mbunge wa Ushetu Emmanuel Cherehani, amesema kiu kubwa ya wananchi wa Jimbo hilo ili kuwa ni madaraja, lakini sasa hivi tatizo hilo serikali inakwenda kulitatua.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, amesema kwa ujenzi wa Madaraja hayo Serikali imewatendea haki wananchi wake.
Meneja Wakala wa Barabara Tanzania (TANDROADS) Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samweli Mwambungu, awali akitoa taarifa ya ujenzi wa Madaraja Matatu katika Halmashauri ya Ushetu, amesema mikataba ya ujenzi wa madaraja hayo ni miezi 12.
Ametaja madaraja hayo kuwa ni daraja la Ubagwe lenye thamani ya Sh.biloni 4.1, daraja la Kasenga bilioni 5.1 na daraja la Ng'wande bilioni 4.1 na kwamba jumla ya gharama zote za ujenzi wa madaraja hayo ni Sh.bilioni 13.5.
Mmoja wa Wakandarasi ambao wanatekeleza ujenzi wa daraja la Ubagwe Godfrey Mbande,kutoka Kampuni ya Salum Motor Trasport Limited, amesema kwamba ujenzi huo watautekeleza ndani ya muda wa Mkataba miezi 12.
Nao baadhi ya wananchi wa Ushetu, wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Madaraja hayo,wakieleza kwamba yatakuwa mkombozi kwao hasa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza katika ziara ya kukagua hatua maendeleo ujenzi wa Madaraja Ushetu.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza katika ziara hiyo.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samweli Mwambungu akitoa taarifa ya ujenzi wa Madaraja Ushetu.
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza na Wakandarasi ambao wanajenga daraja la Ubagwe.
Daraja ambalo wanapita wananchi wa Ubagwe ambalo litafanyiwa ukarabati mkubwa na kuwa daraja la kudumu.
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa wapili (katikati) akiwasili Bugomba Halmashauri ya Ushetu.
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza kwenye Mkutano wa hadhara na wananchi wa Ushetu katika Kijiji cha Bugomba.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kahama Thomas Muyonga akizungumza kwenye mkutano huo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Mboni Mhita akizungumza kwenye mkutano huo.
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa (kushoto)akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.