VIONGOZI WALIOSHINDA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA WAAPISHWA RASMI, RC MACHA AWATAKA WAKAWASOMEE WANANCHI MAPATO NA MATUMIZI

VIONGOZI WALIOSHINDA UHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA WAAPISHWA RASMI, RC MACHA AWATAKA WAKAWASOMEE WANANCHI MAPATO NA MATUMIZI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA
RC Macha.

VIONGOZI wa Serikali za Mitaa ambao wameshinda kwenye uchaguzi uliofanyika novemba 27,wameapishwa Rasmi,huku Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akiwataka viongozi hao, kwenda kuhamasisha shughuli za maendeleo pamoja na kusomea wananchi mapato na matumizi.

Uapisho huo umefanyika leo Novemba 29,2024 katika ukumbi wa mikutano uliopo shule ya Sekondari ya wasichana Shinyanga, iliyopo Mtaa wa Butengwa Manispaa ya Shinyanga.
Macha akitoa nasaha kwa viongozi hao, amewataka wakafanye kazi kwa kuzingatia taratibu na miongozo,pamoja na kuhamasisha shughuli za maendeleo katika maeneo yao, na kuwasomea wananchi mapato na matumizi.

“Nendeni mkafanye mikutano ya kijiji kujadili shughuli za maendeleo, pamoja na kusomea wananchi mapato na matumizi, siyo mnawachangisha wananchi michango harafu hamuwasomei taarifa,hii siyo sawa tena tutakuwa wakali,”amesema Macha.
Amewataka pia viongozi hao wakasimamie pia Amani katika maeneo yao,kuwatambua watu,kuhimiza shughuli za maendeleo,kusimamia miradi,kutatua migogoro ya ardhi,kutunza mazingira,usafi,kupanda miti,kuwasisitiza wananchi wafanye kazi,kuchangia chakula shuleni, pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia mipaka yao.

Amewasisitiza pia wafanye kazi kwa ushirikiano pamoja na viongozi wa vyama pinzani ambao wameshinda kwenye uchaguzi huo na kutobaguana, huku akiwasihi nao viongozi wa upinzani kwamba washirikiane na CCM katika kutekeleza ilani ya chama hicho ambayo kwa sasa ndiyo serikali iliyopo madarakani na siyo kwenda kufanya mapinduzi.
Aidha,ametoa maagizo kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri mkoani humo, kwamba kuanzia mwezi Disemba mpaka Januari 2025, waandae Semina kwa viongozi hao ili wafahamu mambo ya kufanya katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Tunataka viongozi mkawajibike ipasavyo kwa wananchi na siyo kwenda kutumia madaraka yenu vibaya, vyeo ni dhamana na kiongozi atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo ni vyema akajiudhuru na sisi tutafanya uchaguzi mdogo,”amesema Macha.
“Pia mkawe na shughuli za kufanya kama sifa za wagombea zilivyosema kwenye fomu na sitegemei kesho nikutane na kiongozi ambaye atatumia nafasi hiyo kuendesha maisha yake, bali muwe na shughuli zenu za kufanya sababu hamuendi kulipwa mshahara kazi yenu siyo ajira bali mmejitoa kutumikia wananchi,”ameongeza.

Msimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze, amesema uchaguzi huo wa serikali za mitaa umefanyika huru na haki, na kwamba katika Mitaa 55 imechukuliwa yote na CCM, Vijiji 17 navyo CCM, huku Vitongoji 83 vikienda CCM, na kimoja CHADEMA kilichopo Mwagala.
Nao baadhi ya viongozi walioshinda kwenye uchaguzi huo akiwamo Issa Mkondo Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo,na Habiba Jumanne wa Kitangili,wamesema watawatumikia wananchi ipasavyo na kutekeleza ahadi ambazo waliahidi.
Issa Mkondo.
Habiba Jumanne.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umefanyika Novemba 27 mwaka huu, kwa kuchagua Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Mitaa pamoja na wajumbe, ambapo tayari washindi wameshapatikana na wameapishwa.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464