SINA MUHALI NA YEYOTE ANAYECHEZA NA ZAO LA PAMBA - RC MACHA
Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesema kuwa hatokuwa na muhali na mtu yeyote atakayejaribu kucheza au kukwamisha kwa namna yoyote juhudi za kurudisha heshima ya kilimo cha zao la pamba katika Mkoa wa Shinyanga, huku akiwapongeza wananchi, viongozi wa Kijiji cha Mwamishoni Kata ya Bubiki, Jeshi la Polisi na Maafisa kilimo kwa ujumla wao kwa kufanikisha ukamatwaji wa gari hili ambalo lilikuwa na mbegu za pamba, ambazo zilikuwa zikitoroshwa na zilikamatiwa mpaka kati ya Mkoa wa Shinyanga na Mwanza.
RC Macha ameyasema haya tarehe 17 Novemba, 2024 alikuwa akikagua mbegu za pamba ambazo kwa mujibu wa Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) Fraterine Tesha ambaye alimwakilishi RPC Shinyanga SACP Janeth Magomi kwamba mbegu hizi mifuko 107 iliyokuwa imebebwa kwenye gari (FUSO) namba T 618 DRJ ambayo baada ya kukamatwa imehifadhiwa katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Kishapu.
"Sintokuwa na muhali na mtu yeyote ambaye kwa namna moja au nyingine atajaribu kukwamisha juhudi za kurejesha heshimu ya zao la pamba hapa mkoani Shinyanga, na katika hili nitaanza na hawa wote walioshiriki kwenye tukio hili la mbegu za pamba katika Chama Cha Ushirika Mwamishoni hapa Kishapu," amesema RC Macha.
Kando na mifuko 107 ya AMCOS ya Mwamishoni, kulibainika uwepo wa mifuko mingine zaidi yenye takribani Kilo 660 za mbegu za pamba ambazo haifahamiki wamiliki wake baada ya RC Macha kuamuru upekuzi zaidi kati gari hili ambapo zilikutwa chini ya hiyo mifuko 107 ikiwa katika mifupo mchanganyiko.
Kufuatia kugundulika kwa mifuko hii zaidi kumemlazimu RC Macha kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude kuunda Timu maalum kufuatilia, kukagua na kutoa taarifa ya kila AMCOS ilitakiwa kupata mifuko mingapi ya mbegu, imepata mingapi na imebakiwa na mingapi kwa mchanganuo sahihi.
Baada ya sakata hili, kumempelekea RC Macha kwenda kukutana na wananchi wa Mwamishoni ambapo kupitia mkutano wa hadhara amewahakikishia kuwa Serikali yao ipo makini sana na kwamba hata uwepo wa mbegu zinazodhaniwa kuwa siyo halisi ilikwishaanza kulifanyia kazi na sasa matunda yake wameyaona kuwa kumbe mbegu halisia za msimu huu wa 2024/2025 zipo na sasa zitagawiwa kwao bure ili kuhahakisha wakulima wanalima kwa uhakika, kwa tija na kuweza kufikia lengo la kurejesha heshima ya zao la pamba na kuchechemua uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Ikumbukwe kuwa tarehe 10 Novemba, 2024 ndiyo siku aliyofanya ziara ya mwisho wilayani Kishapu iliyodumu kwa siku 6 mfululizo akihamasisha na kufuatilia zao la pamba ambapo kuliibuka hoja uwepo wa mbegu zisizo halisi (Fake) za pamba ambazo zinapelekea wakulima kushindwa kutekeleza vema kilimo cha pamba jambo ambalo aliagiza wataalamu kuchunguza na wampatie taarifa juu ya uwepo wa tetesi hizo ambazo zilionesha kuwa zipo mbegu hakisi (Original) za msimu huu wa 2024/2025 na siyo hizo wanazopewa kwa sasa.
RC Macha amedhamiria kwa chati kabisa kurejesha heshima ya zao la pamba mkoani Shinyanga, zao ambalo limekuwa kimbilio la wakulima walio wengi na ambalo kwa sehemu kubwa limeitangaza vema Shinyanga ndani na nje ya nchi huku likipewa jina la DHAHABU NYEUPE
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464