Msimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze.
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MSIMAMIZI wa uchaguzi Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze,amekanusha kukamatwa kwa kura feki kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura uchaguzi wa serikali za mitaa.
Amebainisha hayo leo novemba 27,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari,kufuatia kuzagaa kwa taarifa kwenye mitandao kuwa baadhi ya vituo vya kupigia kura katika manispaa ya Shinyanga zimekamatwa kura feki.
Amesema uchaguzi wa serikali za mitaa katika manispaa ya Shinyanga,hapa kuwa na kura feki, kama ambavyo taarifa zinavyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
"Uchaguzi wa serikali za mitaa katika Manispaa ya Shinyanga umefanyika huru na haki," amesema Kagunze na kuongeza kuwa
" hapakuwa na kura feki kama alivyodai Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi, sababu mimi nimepita kwenye vituo vyote sijaona hizo kura feki,".
Aidha, amesema katika mitandao ya kijamii,amemsikia pia Ntobi akisema kwamba, licha ya kudai kuwepo kwa kura hizo feki lakini hazikuwekwa kwenye masanduku ya kupigia kura, jambo ambalo Kagunze amesema hali kuathiri uchaguzi huo, na kwamba wagombea waliotangazwa wameshinda kihalali.
Katika hatua nyingine, amesema kwa matokeo ambayo aliyonayo hadi sasa, kwamba Kata 10 kati ya 17, wagombea wote wa CCM pamoja na wajumbe wao wameshinda kwenye uchaguzi huo.
Amezitaja kata hizo kuwa ni Kitangili, Kambarage,Lubaga,Ibinzamata,Ngokolo, Ndala, Masekelo, Mjini, Chamaguha na Ndembezi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Emmanuel Ntobi,amedai kwamba kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura walikamata kura feki, hali ambayo imesababisha uchaguzi kutokuwa huru na haki,ukilenga kuwabeba wagombea wa CCM.