JUMBE AKABIDHI VIFAA VYA MICHEZO KWA WAAMUZI WA MPIRA SHINYANGA

 

Mhandisi James Jumbe Wiswa, mdau mkubwa wa michezo na maendeleo ya jamii, ametimiza ahadi yake ya kusaidia waamuzi wa mchezo wa mpira wa miguu katika Wilaya ya Shinyanga.

 Msaada huu ni sehemu ya kuendeleza michezo na kuhamasisha vipaji vya vijana, ukilenga kusaidia waamuzi wanaoshiriki katika mashindano ya Ligi ya Taifa Wilaya ya Shinyanga.

Vifaa hivyo, vimekabidhiwa kwa niaba ya Mhandisi Jumbe na Masuka Jumbe, leo Novemba 13, 2024, katika Uwanja wa CCM Kambarage,.

Wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Dr. Samia – Jumbe Cup, Mhandisi Jumbe alikubali kutoa msaada huu kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuboresha ufanisi wa waamuzi na wachezaji katika eneo hilo.

Katika hotuba yake, Mhandisi Jumbe alisema, "Wamuzi wa Shinyanga wanapaswa kuona kuwa michezo ni njia muhimu ya kufikia malengo yao maishani. Huu ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika mpira wa miguu wa Shinyanga, na nitatumia kila fursa kuhakikisha vipaji vya vijana wetu vinapata nafasi ya kung'ara."

Viongozi wa Chama cha Wamuzi, akiwemo Joseph Pombe, wamepokea vifaa hivyo kwa furaha na kumpongeza Mhandisi Jumbe kwa msaada huo.

 Wameahidi kutumia vifaa hivyo kutafsiri sheria za mpira wa miguu kwa usahihi na haki, ili kukuza michezo na ufanisi wa waamuzi katika wilaya hiyo.

Mashindano ya Dr. Samia – Jumbe Cup  ni jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya wachezaji na inaendelea kuwa mfano mzuri wa jinsi watu binafsi wanavyoweza kutumia rasilimali zao kuendeleza michezo na kusaidia vijana kufikia malengo yao. Mashindano haya yamekuwa kipengele muhimu cha maendeleo ya michezo katika wilaya ya Shinyanga.

Mhandisi Jumbe amedhihirisha kuwa kuwekeza katika michezo ni kuwekeza katika kizazi kijacho, kwani michezo inatoa fursa ya kukuza vipaji, kukuza nidhamu, na kuhamasisha umoja katika jamii. Kwa juhudi hizi, Shinyanga inakuwa na nafasi kubwa katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

Timu 12 zinazoshiriki mashindano ya mwaka huu ni: Lwambogo FC, Upongoji FC, Original FC, ,Upongoji Star, Qatar FC, Mwadui United, Kitangili United, Rangers FC, Magereza FC, Kambarage Market, na Waha FC

 Mashindano haya yanaendelea kutoa jukwaa la kuwaonyesha wachezaji wa Shinyanga na kuhamasisha maendeleo ya michezo katika mkoa huo.

Soma pia

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464