MADIWANI MSALALA WASHAURIWA KUTOA ELIMU JUU YA MIKOPO ASILIMIA 10 KWA WANANCHI




Mwenyekiti wa Halmashauri Msalala  Mibako Mabubu akiongea kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Na Kareny  Masasy, Kahama 

MKUU  wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga  Mboni Mhita amewataka madiwani watoe elimu juu ya  fedha za mikopo za  asilimia kumi   zinazotolewa kwa wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.

Pia fedha hizo zitakapo tolewa zielezwe  sio za  kuchezea bali  wanapewa  na kurejesha bila riba ili kufanyabiashara na kujiongezea kipato.

Mboni amesema hayo  leo  tarehe 13,Novemba,2024  katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani  kilichofanyika katika halmashauri hiyo nakuhudhuriwa na katibu tawala mkoa .

Mboni amewaomba madiwani wakawe mabalozi  na kutoa elimu juu ya fedha hizo ili kusiwepo na dosari ya wananchi  watakao anza  kukopa nakushindwa kurejesha .

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mibako  Mabubu amesema  suala la kuongeza umri wa ukopaji kwa kundi la vijana kutoka miaka 35 hadi 45  limewafurahisha  sana.

“Umri wa  kuanzia miaka 18 hadi  35 vijana hao walikuwa wakisumbua hata katika urejeshaji wao hivyo  kuongezeka kwa umri  wa vijana  kukopa watapata  nidhamu ya fedha wanayokopeshwa”amesema Mabubu.



Mwenyekiti wa halmashauri hiyo amezishauri taasisi  za serikali  zinapotekeleza majukumu yao  na kuitwa kwenye vikao vya baraza au  kamati wasisite kuhudhuria kwani wakifanya hivyo wanapunguza maswali kwa madiwani.

Diwani wa kata ya Ikinda Matrida Musoma ameipongeza halmashauri kwa kitendo cha ukusanyaji wa mapato  kwa mwaka wa fedha 2024/2025 cha  robo ya kwanza kufikia zaidi ya  asilimia 36.

Diwani wa kata ya Mwakata  Ibrahimu  Six  ambaye ni makamu Mwenyekiti  alimuomba  mkuu wa wilaya  Mboni Mhita  kuangalia uwezekano wa kutenganishwa  Mageti  mawili yaliyowekwa karibu  kwaajili ya ukusanyaji ushuru eneo la Isaka.

Six amesema  kazi nzuri imefanywa na kamati ya fedha ,uongozi na Mipango kwa kushirikiana na wataalamu  hadi kufikia  zaidi ya asilimia 36 ya ukusanyaji wa mapato karika robo ya kwanza kwa mwaka huu.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464