MADIWANI WALIA NA MIUNDOMBINU YA BARABARA, IKIWEMO UKOSEFU WA MAJI SAFI NA SALAMA

Mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu William Jijimya akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani 

Suzy Butondo, Kishapu Shinyangapress blog

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Kishapu Mkoani Shinyanga wamesema hali ya miundombinu ya barabara katika kata zao ni mbaya, ambazo katika msimu huu wa mvua barabara hizo zisipotengenezwa zinaweza zisipitike hivyo wameiomba serikali ifanye haraka ili waweze kuondokana na adha hiyo.

Licha ya changamoto hizo pia wamesema baadhi ya kata zao wanashida ya maji, ambapo kata ya Masanga na kata ya Ndoleleji kuna shida kubwa ya maji na tatizo kubwa ni mkandarasi ambaye anatekeleza mradi wa maji katika kata hizo, ambapo maeneo ya vyanzo vya maji bado hajakamilisha na alisaini mkataba toka mwaka jana.

Hayo wameyasema leo Novemba 5,2024 wakati wakitoa taarifa za kata zao katika kikao cha baraza, ambapo wamesema wanachangamoto ya maji na hali ya barabara zao ni mbaya hivyo ni vizuri serikali ikachukua hatua za haraka ili zinaponyesha mvua zikute barabara zimeshatengenezwa.

Diwani wa kata ya Masanga Enock Reuben Iakizungumzia changamoto ya maji amesema,wananchi wanapata shida kubwa ya maji, huku mkandarasi ambaye anatekeleza mradi huo amesaini mkataba wake toka mwaka jana lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea, hivyo wanashindwa kumuelewa ni kwa nini hafanyi kazi ipasavyo ili wananchi waondokane na adha ya maji.


"Kwa kweli mkandarasi huyu ameonekana kushindikana,lakini pia ameonekana kuwa na nguvu zaidi ya serikali, hivyo niombe baraza hili mtusaidie tunaomba aitwe aje ahojiwe kesho na baraza hili, ili ajibu ni lini atatekeleza mradi wa maji ili wananchi waondokane na adha hiyo kwani mpaka leo maeneo ya vyanzo vya maji hayajaanza kutekelezwa na tayari maji yameshaingia mtoni lakini hatuoni kinachoendele ."amesema Enock

Diwani wa kata ya Ndoleleji Mohamed Amani amesema kwa kweli mkandarasi huyo amegeuka kuwa kelo kubwa kwa wananchi, hivyo anatakiwa kuitwa aje ahojiwe mbele ya baraza hili aseme anashida gani mpaka ashindwe kumalizia mradi huo.

"Mkandarasi huyu toka asaini mkataba leo ana mwaka mzima kaweka mabomba viunganishi, aliambiwa maji yaunganishwe mwezi wa tisa lakini mpaka leo hatumuoni na hajafanya chochote aje hapa aseme anashida gan"alihoji Amani.

Diwani wa kata ya Ngofila Nestory Ngude akizungumzia barabara amesema miundombinu ya barabara katika kata yake hairidhishi, kwani barabara nyingi ni mbovu, hivyo ameiomba serikali itengeneze barabara hizo kwani wananchi wanapata shida wanapohitaji kuvuka kwenda eneo jingine kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

"Sisi kilio chetu kikubwa ni barabara hasa ya kutoka Inolelo kwenda Miyuguyu ni mbovu sana niwaombe wataalamu mlifanyie kazi hilo kabla ya mvua kuanza kunyesha kwani hali ni mbaya kwani mvua zikinyesha barabara hizo hazitapitika tena,"amesema Ngude.

"Changamoto nyingine ni kukosekana kwa maji safi na salama, wananchi wanapata shida sana tunaomba serikali ilisimamie na kata yangu iweze kupata maji safi na salama ili kuepuka magonjwa ya kuhara "amesema Ngude

Aidha Ngude amesema changamoto nyingine katika kata yake ni upungufu mkubwa wa nyumba za walimu katika shule za msingi, pamoja na madawati wanafunzi wengi wanakaa chini, hivyo ameiomba serikali iwaletee madawati na kuleta walimu wa kutosha latika shule za msingi kata ya Ngofila.

Diwani wa kata ya Bubiki James Kasomi amesema changamoto kubwa katika kata yake ni kutokuwa na kituo cha afya licha ya wananchi kuchangia jengo na kujenga boma ambalo limeshafikia kufungwa lenta, uchakavu wa shule ya Mwamishori ambapo madarasa yale yanatishia uhai wa wanafunzi wakiwa shuleni,.

"Changamoto nyingine ni ujenzi wa vyumba vya walimu katika shule ya msingi ya ushirika hakuna hata nyumba moja ya mwalimu walimu hao wanapata shida hivyo wanaiomba serikali ilifanyie kazi ili changamoto hizo ziondolewe ,"amesema Kasomi.

Diwani wa kata ya Kiloleli Edward Manyama amesema barabara ya kutoka Kiloleli kwenda Muguda na barabara ya kutoka Muguda kwenda Jijongo imekatika kwa mvua za masika zilizopita, amromba asaidiwe na wataalamu wa kutoka ofisi ya Tarura ni lini barabara hizo zitajengwa.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Kishapu Emmanuel Johnson akijibu hoja za madiwani katika suala la nyumba za walimu amewaomba madiwani waendelee kuwahamasisha wananchi waanzishe kujenga maboma,kwani serikali itaendelea kushirikiana na wananchi.

"Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza bajeti kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara, ambapo baadhi zitajengwa kwa kiwango cha lami, na wakandarasi wataanza kazi hivi karibuni ili kuhakikisha barabara zetu zinapitika,"amesema Johnson.


"Hivyo nakubaliana na wajumbe kesho awepo mkandarasi wa mradi wa maji na wataalamu wa Tarura na Ruwasa kwa ajili ya kujibu hoja hizi,, kwani katika mradi wa maji mkandarasi alishasaini mkataba tayari kwa kuanza kazi"ameongeza.

Aidha mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu William Jijimya amesema kweli wananchi wanashida ya barabara na maji lakini kesho wakuu wa Taasisi za maji na barabara watakuwepo hapa kwa ajili ya kujibu hoja hizi, ili watoe mikakati ya kutatua changamoto mbalimbali za wananchi.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Kishapu, Piter Mashenji katika kikao hicho  amewataka watendaji wa halmashauri hiyo kuchukua hatua za haraka katika kushughulikia changamoto hizo, ili kujibu hoja za wananchi na kuhakikisha maendeleo ya kila kata yanaonekana.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Kishapu Emmanuel Johnson akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani 
Mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu William Jijimya akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani 
Watumishi wa halmashauri ya kishapu wakifatilia mahojiano kwenye Baraza la madiwani
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakifuatilia makabrasha 

Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakifuatilia makabrasha 
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakiwa kwenye kikao cha  baraza la madiwani
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakiwa kwenye kikao cha  baraza la madiwani
Wakuu wa idara wa halmashauri ya Kishapu wakiwa kwenye baraza la madiwani
Wakuu wa idara wa halmashauri ya Kishapu wakiwa kwenye baraza la madiwani
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakiwa kwenye kikao cha  baraza la madiwani
Diwani wa kata ya Talaga Richard Dominiko akizungumza kwenye kikao cha baraza hilo
Diwani wa kata ya Bubiki James Kasomi akito taarifa ya kata yake kwenye kikao cha baraza hilo
Diwani wa kata ya Ngofila Nestory Ngudeitoa taarifa ya kata yake
Diwani wa kata ya Kiloleli Edward Manyama akizungumza kwenye baraza hilo
Diwani wa kata ya Masanga Enock Reuben akizungumza 
Diwani wa kata ya Ndoleleji  Mohamed Amani akizungumza
Katibu wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Kishapu Piter Mashenji akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani 























Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464