TAMCODE YAWAASA WASANII WA SANAA NA UTAMADUNI KUINGIA MIKATABA YENYE TIJA

Kikundi cha ngoma ya kabila la Wafipa cha Mama Chanje wakionyesha Manjonjo yao ya kucheza ngoma zenye ujumbe mbalimbali mjini Sumbawanga, Rukwa, Tanzania hivi karibuni. 

Wasanii wanaofanya kazi kwenye sekta ya Urithi wa Utamaduni Usioshikika wameaswa kuingia mikataba yenye tija na wateja na kujua stahiki zao kabla ya kwenda kufanya kazi kokote ili kujikwamua kiuchumi.

Wasanii hao pia wameaswa kunadi kazi zao mitandaoni ili waweze kupata fursa ya kufanya kazi ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa leo mjini Bagamoyo na Mkurugenzi wa TAMCODE, Rose Ngunangwa  wakati akitoa uzoefu wa shirika lake katika kutumia redio za jamii na vyombo vya kidijitali katika kukuza na kulinda Urithi wa Utamaduni Usioshikika katika Mikoa ya Rukwa na Katavi.

Mdahalo huu ulifanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo na uliandaliwa na Serikali pamoja na UNESCO ili kuwajengea uelewa vijana kujua namna namna ya kulinda na kukuza Utamaduni Usioshikika katika zama za kidijitali.

Akiongea katika mdahalo huo, Bi Ngunangwa alitoa uzoefu waliopata Mkoani Rukwa na kusema alikutana na kikundi cha ngoma ambacho licha ya kuanzishwa mwaka 1965 wasanii wake walikuwa bado hawajanufaika na kazi zao.

“Wasanii wa kikundi cha Mama Chanje Sumbawanga walitujuza kuwa kuna wakati wanaitwa kufanya kazi miji ya mbali kama Dodoma ambapo hupewa chakula, usafiri na malazi na kuishia kuambulia fedha kiduchu ambazo hazikidhi kitu, alisema.

Bi Ngunangwa alisisitiza kwamba wasanii hao wanapopata fursa kamwe wasikimbilie kukubali tu kuona miji kwani kuna maisha baada ya wao kula na kulala.

“ Urithi wa Utamaduni Usioshikika ni fursa, ni ajira, ni kipato na uhai,” alisema.

Kwa upande wake, Nyakanga Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bi. Hadija Shabani alisema mara nyingi wao hufanya kazi wakiwa watatu ambapo hupewa shilingi elfu hamsini tu kiwango ambacho huwafanya wasisonge mbele kimaisha.

Mjadala wa leo umetufungua macho nasi tutayatumia maarifa hayo katika kazi zetu ili kuboresha kipato,” alisema Nyakanga huyo ambaye anatajwa kama Maktaba inayotembea kutokana na ujuzi wake.

Akichangia mjadala huo, Msanii maarufu wa kikundi cha ngoma ya Mdundiko, Madogoli na Vanga mjini Bagamoyo bwana Mpazi Kazi alisema licha ya kufanya kazi nyingi zinazotambulika ameishia kupata jina kubwa ambalo haliakisi kipato anachopata.

Alikiri kuwa amepata moyo sana na kuanzia sasa atatumia elimu aliyopata ili kikundi chake kiweze kujikwamua kiuchumi.

Wito huu unakuja huku kukiwa na malalamiko mengi ya wadau kutumia vikundi vya sanaa katika shughuli mbalimbali na kutoa ujira mdogo huku baadhi wakitoa chakula na pombe tu kama ujira.

Mjadala huo uliwakutanisha wadau wa sekta hii wakiwemo wazee maarufu na wazee wa mila, asasi za kiraia, Manyakanga maarufu, Wasanii wa Ngoma, Maofisa utamaduni, wanafunzi wa chuo cha TASUBA, wahadhiri na watendaji wa serikali kutoka Bara na Zanzibar.

Urithi wa Utamaduni usioshikika unajumuisha maarifa, uzoefu na ujuzi wa kipekee wa kujieleza katika jamii husika ikiwemo lugha, uwezo wa kughani mashairi ngonjera, nahau, ngoma za asili, ujuzi wa asili wa kupika vyakula vya asili na kutengeneza vitu mbalimbali vya kiutamaduni.

Urithi huu pia unajumuisha michezo ya kiasili kama bao, solo, rede, mdako, mbio za magunia pamoja na mengineyo.
Kikundi cha ngoma ya kabila la Wafipa cha Mama Chanje wakionyesha Manjonjo yao ya kucheza ngoma zenye ujumbe mbalimbali mjini Sumbawanga, Rukwa, Tanzania hivi karibuni.
Kikundi cha ngoma ya kabila la Wafipa cha Mama Chanje wakionyesha Manjonjo yao ya kucheza ngoma zenye ujumbe mbalimbali mjini Sumbawanga, Rukwa, Tanzania hivi karibuni.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464