BENKI YA CRDB YASHINDA TUZO YA KIMATAIFA YA BENKI BORA TANZANIA 2024

  

Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (wapili kushoto) akiwa na tuzo ya Benki Bora Tanzania kwa mwaka 2024 ambayo benki hiyo imetunukiwa katika tuzo za taasisi bora za fedha duniani za “The Banker” zinazotolewa na gazeti la Financial Times la nchini Uingereza. Wengine pichani ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Benki ya CRDB, Emmanuel Kiondo (wapili kulia), Mhariri Mkuu wa Jarida la The Banker Silvia Pavoni, na Mwandishi Nguli wa Habari wa nchini Uingereza, Sir Trevor Lawson McDonald.

---------
London, Uingereza. Tarehe 4 Desemba 2024: Benki ya CRDB imetangazwa kuwa benki bora zaidi Tanzania kwa mwaka 2024 katika tuzo za taasisi bora za fedha duniani za “The Banker” zinazotolewa na gazeti la Financial Times la nchini Uingereza.

Tuzo hii iliyopokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa aliyeongozana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Emmanuel Kiondo, ni muendelezo wa Benki ya CRDB kutambulika kimataifa baada ya kushinda tuzo ya benki bora kwa biashara ndogo na za kati Tanzania iliyotolewa na Jarida la Euromoney la Uingereza pamoja na benki bora Tanzania, benki benki bora kwa biashara ndogo na za kati Tanzania na programu (mobile application) bora ya benki zilizotolewa na Jarida la Global Finance la nchini Marekani mapema mwaka huu.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Tully Esther amesema ni furaha kuona dunia inatambua kinachofanywa na Benki ya CRDB ambayo kila siku inazidi kukua kutokana na kuwahudumia wateja wake kwa viwango vya kimataifa.

“Kushinda tuzo ya The Banker kunadhihirisha mchango wetu wa kuwa benki kubwa zaidi nchini na nje ya mipaka yetu. Tuzo hii imetambua kazi kubwa inayofanywa na wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB tukishirikiana na wabia wetu wa kimkakati katika kutoa huduma bunifu zinazotatua changamoto za wateja wetu pamoja na kuchangia maendeleo endelevu ya jamii yetu,” amesema Tully Esther.

Kwa mwaka 2023, taarifa za fedha za Benki ya CRDB zinaonyesha thamani ya mali zake imeongezeka kwa asilimia 14.48 na kufika shilingi trilioni 13.32 huku mtaji wake ukipanda kwa asilimia 20.4 na kufika shilingi trilioni 1.78. Katika kipindi hicho, Benki ya CRDB ilipata faida ya shilingi bilioni 422.79 baada ya kodi.

Benki pia imetanua huduma zake nje ya mipaka ya nchi kwa kufungua tawi nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Congo huku ikimarisha mtandao wake nchini kwa kufikisha zaidi ya matawi 260 yanayowahudumia wananchi katika halmashauri zote.

Tully Esther amesema Benki ya CRDB pia imekuwa ikibuni huduma na bidhaa zake kwa kutumia teknolojia ili kuendana na mabadiliko yanayotokea ulimwenguni akitolea mfano jukwaa la SimBanking linaloongoza kwa ubora wa huduma za benki kiganjani pamoja na TANQR inayowaruhusu wateja kufanya malipo kidijitali iwe kwenda katika akaunti ya benki au akaunti ya simu ya mkononi.

“Sera ya benki yetu pia ni kulinda mazingira. Mwaka jana tuliitambulisha Hatifungani ya Kijani ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kutekeleza miradi yenye mrengo wa kulinda mazingira. Hatifungani hii ilikuwa ya kwanza kubwa zaidi Kusini mwa Jangwa la Sahara,” amesema Bi. Tully Esther.

Mafanikio hayo yaliyofikiwa na Benki ya CRDB ni sehemu ya vigezo vilivyoipa ushindi wa benki bora Tanzania katika tuzo za “The Banker” ambazo hushirikisha mataifa 120 zikwajumuisha wataalamu wenye uzoefu na mchango mkubwa kwenye sekta ya benki, benki za biashara na taasisi ndogo za fedha ambazo hushindanishwa kupima ubora wa huduma zao. Majaji hupima kazi za washindani kwa zaidi ya miezi mitano na kutumia vigezo maalumu kumpata mshindi aliyetoa huduma borandani ya miezi 12 iliyopita.

Kwa Benki ya CRDB kushinda tuzo hii, kunaonyesha namna Tanzania inavyokuza ushawishi wake katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na sera nzuri za fedha ilizonazo. Kwa miaka kadhaa sasa, Tanzania imekuwa ikitekeleza sera na mikakati ya kuwajumuisha wananchi katika huduma za fedha ili kuwa na uchumi jumuisha suala ambalo Benki ya CRDB inalitekeleza kila uchwao.

“Mazingira haya pamoja na uchumi imara unaokua kwa kasi nzuri, yanalifanya taifa letu kuwa la mfano katika ubunifu kwenye ukanda huu jambo linalowavutia wawekezaji wa ndani na nje kuje kuzichangamkia fursa zilizopo,” amesisitiza Tully Esther. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464