CHUO CHA SAYANSI ZA AFYA KOLANDOTO KIMEADHIMISHA MIAKA 63 YA UHURU KWA KUPANDA MITI
CHUO cha Sayansi za Afya Kolandoto katika Manispaa ya Shinyanga, kimeadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanzania Bara kwa kupanda miti kwenye maeneo ya chuo hicho.
Zoezi hilo la upandaji miti limefanyika leo Desemba 10,2024 likiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Mipango,Fedha na Utawala,Michael Henerico.
Henerico akizungumza mara baada ya zoezi la upandaji miti kukamilika,amesema jana ilikuwa ni siku ya kumbukizi ya nchi kupata uhuru Desemba 9, na kwamba wao wameamua kuadhimisha leo kwa kupanda miti katika maeneo ya chuo hicho ili kutunza mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,pamoja na kupendezesha madhari ya chuo.
“Leo tumepanda miti 200 katika maeneo yetu ya hapa chuoni, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanzania Bara,”amesema Henerico.
Msimamizi wa Mazingira chuoni hapo Josephine Charles, amesema, wamekuwa na tabia ya kupanda miti mara kwa mara ili kutekeleza maagizo ya viongozi ya utunzaji wa mazingira pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, na kwamba April mwaka huu, walipanda miti 150 na yote inaendelea vizuri na leo wamepanda tena miti 200.
Amesema wamekuwa wakipanda miti ya kivuli, matunda na mapambo, na kwamba mwakani 2025 wanatarajia kuanzisha vitalu vya miche, ili wawe mabalozi wazuri wa utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ikizingatiwa Mkoa wa Shinyanga unakabiliwa na hali ya ukame.
Mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho Magreth Milimo, amesema upandaji huo wa miti una faida kwao, na kwamba licha utuzaji wa mazingira pia watapata kivuli kwa ajili ya kujisomea na kufanya vizuri katika masomo yao.
Aidha, jana Desemba 9 ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara, ambapo mikoa mbalimbali iliadhimisha siku hiyo, huku wengine wakifanya shughuli za kijamii.
Kauli mbiu ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara inasema:Uongozi Madhubuti na Ushirikishwaji Wananchi ni Msingi wa Maendeleo.
TAZAMA PICHA👇👇
Makamu Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto,Mipango,Fedha na Utawala, Michael Henerico akizungumza kwenye zoezi hilo la upandaji miti.
Msimamizi wa Mazingira Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Josephine Charles akizungumza.
Mwanafunzi Magreth Milimo akizungumza.
Msimamizi wa Mazingira Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Josephine Charles akitoa maelekezo namna ya kupanda mti.
Msimamizi wa Mazingira Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto Josephine Charles akipanda mti.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto,mipango,fedha na utawala, Michael Henerico akipanda mti.