MAAFISA USAFIRISHAJI SHINYANGA WAPEWA ELIMU KUDHIBITI AJALI ZA MWISHO WA MWAKA

MAAFISA USAFIRISHAJI SHINYANGA WAPEWA ELIMU KUDHIBITI AJALI ZA MWISHO WA MWAKA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MAAFISA usafirishaji katika Manispaa ya Shinyanga, wamepewa elimu ya kuzingatia sheria za usalama barabara, ili kudhibiti ajali ambao zimekuwa zikitokea kuelekea mwisho wa mwaka na kuukaribisha mwaka mpya, huku wakionywa pia kuacha tabia ya kubebesha wanafunzi juu ya mapaja ya abiria wanaume.
Elimu hiyo imetolewa leo Desemba 12,2024, na Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma kutoka Trafiki Makao Makuu (ACP) Michael Deleli Stephen, katika ukumbi wa Bwalo la Polisi Manispaa ya Shinyanga.

Amesema Jeshi la Polisi linatambua umuhimu wa maafisa usafirishaji na lipo bega kwa bega nao, na ndiyo maana imekuwa ikitoa elimu ya mara kwa mara, kuwakumbusha juu ya kutii na kuzingatia sheria za usalama barabarani, ili kudhibiti ajali zisizo za lazima zitokanazo na uzembe wa dereva.
“Sasa hivi tunaelekea kufunga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya 2025, hivyo ni maafisa usafrishaji lazima muwe makini na matumizi ya barabara, ili kudhibiti ajali na kuumaliza mwaka salama,”amesema ACP Stephen.

Aidha,ametaja mambo ambayo madereva hao ambayo wanapaswa kuzingatia ili kutii sheria za usalama barabarani, kuwa ni wavae kofia ngumu,kutoendesha mwendokasi,kuzidisha abiria, na ku-“ovetake” hovyo,pia amewasisitiza wawe wana vaa sare,kuwa na lessen pamoja na vyombo vyao kuvikatia bima.
Katika hatua nyingine, amewaonya maofisa hao,kwamba wajihadhari pia na ukatili wa kijinsia, kwa kutoshika hovyo wanawake kwenye maungo yao, kutongoza wake za watu, na wafanyakazi majumbani wanapotumwa kupeleka mboga, na kuacha pia kuwabebanisha wanafunzi juu ya mapaja ya wanaume.

Kaimu Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Shinyanga SP Methew Ntakije, naye amesisitiza juu ya uzingatiwaji wa sheria za usalama barabara, hasa kwa madereva wa bodaboda ambao wamekuwa wakiweka kofia ngumu chini ya miguu badala ya kuzivaa kichwani, na kwamba watakao kamatwa watachukuliwa hatua.
Mkuu wa Polisi jamii Mkoa wa Shinyanga (ACP) Fraterine Tesha,amesihi pia Maafisa hao usafirishaji, kwamba wanapokuwa katika majukumu yao, washirikiane na Askari Kata katika kuripoti vitendo vya uhalifu.

Nao Maafisa hao usafirishaji, wameshukuru kupewa elimu hiyo na kuahidi kutii sheria za usalama barabara, ili kudhibiti kukithiri kwa ajali, hasa kuelekea kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka.

TAZAMA PICHA 👇👇
Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma kutoka Trafiki Makao Makuu (ACP) Michael Deleli Stephen,akitoa elimu kwa Maafisa usafirishaji Manispaa ya Shinyanga.
Kaimu Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Shinyanga SP Methew Ntakije, akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Polisi jamii Mkoa wa Shinyanga (ACP) Fraterine Tesha, akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Madereva wa Bodaboda wilaya ya Shinyanga Mohamed Marabu akitoa shukani kupewa mafunzo hayo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464