WANANCHI MWAMALASA WAFUNGUKA MATUKIO YA UKATILI, MDAHALO WA HELP AGE TANZANIA
SHIRIKA la Help Age Tanzania, limeendesha mdahalo na wananchi wa Kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu, kujadiliana na kuweka maadhimio juu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, watoto, wazee, watu wenye uemavu, ndoa za utotoni, na kusaidia kuimarisha ushiriki wa wanaume katika masuala ya Afya ya uzazi na haki.
Mdahalo huo umefanyika leo Desemba 14,2024 katika Kijiji cha Mwamalasa, ulioshirikisha makundi rika yakiwamo ya vijana,wanawake,mabinti wazee,watu wenye ulemavu,viongozi wa dini,Maofisa Maendeleo, Mtendaji wa Kata ya Mwamalasa, pamoja na dawati la msaada wa ngazi ya Halmashauri, ili wajadili ukatili uliopo kwenye Kata hiyo na namna ya kuchukua hatua kuudhibiti ikiwamo kuweka maadhimio.
Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Shirika la Help Age Tanzania John Eddy, amesema mdahalo huo ni utekelezaji wa mradi wa chaguo langu haki yangu, ambao unafadhiliwa na serikali ya Finland kupitia Shirika la UNFPA,kwa mgawanyo wa majukumu na kwamba Help Age imekasimishwa eneo la kuendesha kwa wanaume,vijana, na jamii kwa ujumla ili kubadilisha mitazamo,na fikra katika kupunguza ukatili ndani ya jamii na kuimarisha ushiriki wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na haki.
“Mradi huu wa chaguo langu haki yangu, hapa Kishapu tunatekeleza katika Kata 7, ambazo ni Mwamalasa, Mwamashele, Lagana, Taraga, Idukilo, Ukenyenge na Mwaweja,”amesema Eddy.
Nao wananchi wa Mwamalasa wakijadili kwenye mdahalo huo, wamebainisha baadhi ya vitendo vya ukatili, kuwa ni kukithiri kwa vipigo kwa wanawake, watoto, na wanafunzi kuozeshwa ndoa za utotoni.
Mmoja wa wananchi hao Benard Jitindi,amesema watoto wa kike wamekuwa wakinyimwa fursa za kupata elimu, ambapo wazazi wamekuwa wakiwaozesha ndoa za utotoni kwa tamaa ya kupata mali.
Binti Rebeka Nkuba, ametaja sababu nyingine ambayo imekuwa ikisababisha wanafunzi kupewa mimba za utotoni, kuwa ni kusoma shule umbali mrefu, ambapo njiani hukutana na vishawishi na kuishia kupewa ujauzito na kuacha masomo.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamalasa Festo Daudi, amesema kwamba kijijini humo kuna vitendo vingi vya ukatili, lakini jamii imekuwa waoga kutoa taarifa na kukumbatia vitendo hivyo.
Ametolea mfano kwamba, kuna Mwanamke Mmoja ambaye ana mtoto mchanga wa miezi miwili, alipigwa na mumewake hadi kuvunjika mkono, lakini familia yake ilificha tukio hilo, huku mhanga mwenyewe alipohijiwa alikana, na kutoa sababu zingine za yeye kuvunjika mkono ambazo ni uongo.
Amesema kunatukio jingine la Mtoto kufungwa Kamba na Mjomba wake kisa kula biskuti, huku akitishiwa kuchomwa visu hadi afe, lakini anashukuru alipata taarifa mapema na kufika eneo la tukio na kumuwahi mtoto huyo.
Afisa Maendeleo ya jamii wilayani Kishapu Efrem Kilango, ameitaka jamii kwamba wasikae kimya wanapokuwa wakiona matukio ya ukatili, bali watoe taarifa ili wahusika wachukuliwe hatua na kukomesha vitendo hivyo.
Mtendaji wa Kata ya Mwamalasa Masoud Upanga, amesema kwamba licha ya kwamba Kata hiyo ni kituo chake kipya cha kazi, ameahidi kwamba vitendo vyote vya ukatili ambavyo vimebainishwa na wananchi, kwamba atavifanyiwa kazi, huku akiomba ushirikiano kwa jamii kutoa taarifa na kuwa tayari kutoa ushahidi.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Shirika la Help Age Tanzania John Eddy akizungumza kwenye mdahalo huo.
Afisa Maendeleo ya jamii wilayani Kishapu Efrem Kilango akizungumza kwenye mdahalo huo.
Mtendaji wa Kata ya Mwamalasa Masoud Upanga akizungumza kwenye mdahalo huo.
Majadiliano yakiendelea.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464