RC MACHA AZINDUA KITUO CHA HUDUMA JUMUISHI WILAYANI KISHAPU “ONE STOP CENTER”
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amezindua Rasmi Kituo cha Huduma Jumuishi “One Stop Center” wilayani Kishapu,kwa ajili ya kuhudumia Wahanga wa matukio ya ukatili wa kijinsia,huku akisisitiza kuwepo na usiri dhidi ya taarifa za Wahanga wa ukatili.
Hafla ya uzinduzi wa kituo hicho imefanyika leo Desemba 16,2024, ambapo jengo lake limejengwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu(UNFPA) linaloshughulikia Afya ya uzazi, kwa ufadhili wa Finland, kupitia mradi wa UNFPA unaoitwa Chaguo langu Haki yangu.
Macha akizungumza kwenye hafla hiyo, kwanza amewapongeza wafadhili hao kwa ujenzi wa Kituo hicho,huku akiwasihi wananchi wakitumie vizuri katika masuala mazima ya vitendo vya ukatili, ili haki ipatikane na kutokomeza vitendo hivyo ndani ya jamii.
“tujitokeze kukitumia Kituo hiki cha huduma jumuishi ,msimalizane masuala ya ukatili wa kijinsia majumbani hasa ya ubakaji watoto, akina mama fikeni kituoni hapa kutoa taarifa za kufanyiwa ukatili, na wanaume vilevile mtoe taarifa na kupatiwa huduma,”amesema Macha.
Amewasihi pia Watumishi wa Kituo hicho, kwamba wanapohudumia Wahanga wa matukio ya ukatili, wawe wanatunza siri, huku akisisitiza juu ya utunzwaji wa jengo hilo pamoja na kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara na kuwekwa katika mazingira mazuri.
Amekemea pia ukatili mpya ambao umekuwa ukifanywa na akina mama, kwa kuweka watoto mbele ya tenki la mafuta kwenye bodaboda hali ambayo ina hatarisha afya zao.
Katika hatua nyingine, amewasihi wazazi kwamba mwezi januari mwakani 2025, kwa wale watoto ambao wamefikia hatua ya kuanza shule wawapeleke kuanza masomo,na upande wa Secondari wanafunzi wote waliofaulu nao wapelekwe shule.
Amekemea pia vitendo vya baadhi ya wazazi kuwaficha watoto wenye ulemavu na kuwanyima haki yao ya kielimu, kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua kali, sababu serikali itaendesha msako wa nyumba kwa nyumba.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Dk. Godfrey Kisusi, awali akisoma taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho, amesema kimeanza kujengwa Agosti 30/2023, na kukamilika Marchi 15,2024, na kwamba awamu ya kwanza walipewa sh.milioni 117, awamu ya pili milioni 20,awamu ya tatu milioni 41.2 kwa ajili ya kukamilisha kila kitu na kuanza kutoa huduma.
“Takwimu za matukio ya ukatili kuanzia Marchi hadi Desemba 2024, yametokea matukio 192, yakiwamo ya kimwili, ngono, kisaikolojia na utelekezaji watoto,”amesema Dk.Kisusi.
Amesema kituo hicho cha huduma jumuishi kimesaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma stahiki kwa Wahanga wa matukio ya ukatili pamoja na usiri, huku akiwasihi wananchi wawe wanatoa taarifa mapema za matukio hayo ndani ya masaa 72 ili wahanga wapate huduma haraka.
Dk.Kisusi amebainisha changamoto ambazo bado zinawakabili, kuwa ni ukosefu wa nyumba salama kwa ajili ya kuhifadhi Wahanga wa ukatili hasa watoto ambao upewa mimba za utotoni, sababu wakirudi kwa wazazi wao hurubuniwa na kuharibu ushahidi kwa kuwakana Watuhumiwa.
Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA Tanzania Mark Bryan Schreiner, amesema Kituo hicho kitakuwa na msaada mkubwa katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, katika utoaji wa huduma kwa Wahanga wa ukatili.
“Kama tunavyofahamu sote hapa Tanzania, kama ilivyo katika nchi nyingi duniani, wanawake na wasichana wanaishi kwa hofu ya unyanyasaji, ambapo asilimia 23 na asilimia 6.1 ya wanawake na wasichana mkoani Shinyanga wenye umri wa miaka 15 hadi 49, wamekumbana na ukatili wa kimwili na kigono unaofanywa na wanandoa au mtu mwingine, kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita kwa mujibu wa TDHS 2022,”amesema Mark.
Ameongeza kuwa pia asilimia 46 ya wanawake wenye umri wa miaka 20-24 mkoani Shinyanga, waliolewa wakiwa na umri wa miaka 18.
Pia, Mark ametoa shukrani kwa serikali ya Finland, kwa ufadhili wa mradi wa Chaguo langu Haki yangu, ambao UNFPA wanautekeleza katika mikao ya Mara na Shinyanga, kupitia mashirika ya WILDAF, Help Age Tanzania, Interfaith Partnership,TGNP na C-Sema.
Naye Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Finland Tanzania Juhana Lehtinen, amesema wataendelea kushirikiana na serikali hapa nchini katika mapambano ya kupinga vitendo ya ukatili wa kijinsia, na kwamba Kituo hicho cha huduma jumuishi,kitasaidia wanawake na watoto dhidi ya kupambana na ukatili na kuleta usawa wa kijinsia.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu, amepongeza ujenzi wa Kituo hicho, na kuahidi kwamba Jengo hilo watalitunza
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Kituo cha huduma jumuishi (One Stop Center) wilayani Kishapu.
Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA Tanzania Mark Bryan Schreiner,akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Kituo cha huduma jumuishi (One Stop Center) wilayani Kishapu.
akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Kituo cha huduma jumuishi (One Stop Center) wilayani Kishapu. akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Kituo cha huduma jumuishi (One Stop Center) wilayani Kishapu..
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Dk. Godfrey Kisusi, akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha 0kushoto)akizundua Kituo cha huduma Jumuishi wilayani Kishapu (kulia) ni Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA Tanzania Mark Bryan Schreiner
Picha ya pamoja
uzinduzi wa Kituo cha huduma Jumuishi ukiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464