RC MACHA AWAONYA WENYEVITI WA VIJIJI,VITONGOJI MATUMIZI MABAYA YA MIHURI KUJIPATIA MAPATO AMBAYO SIYO HALALI


RC MACHA AWAONYA WENYEVITI WA VIJIJI,VITONGOJI MATUMIZI MABAYA YA MIHURI KUJIPATIA MAPATO AMBAYO SIYO HALALI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amewaonya wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji Halmashuri ya Shinyanga,kwamba wasitumie Mihuri vibaya kuendekeza masuala ya rushwa na kujipatia mapato ambayo siyo halali.

Amebainisha hayo leo Desemba 18,2024 wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, namna ya utekelezaji wa majukumu yao katika kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.
Amesema baadhi ya viongozi waliochaguliwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27,2024 ni wapya,hivyo wameona ni vyema kuwapatia mafunzo, ili wakawe wazalendo na waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao, na wasitumie Mihuri vibaya na kuendekeza Rushwa.

"Nawapongeza kwanza kwa kuchaguliwa na wananchi,hivyo nendeni mkawe Wazalendo,na Waadilifu katika kuwatumikia wananchi na msitumie mihuri vibaya kwa kuendekeza Rushwa na kujipatia mapato ambayo siyo halali," amesema Macha.
Amesewasihi pia kusimamia Amani na ulinzi katika maeneo yao ikiwamo kudhibiti uharifu, kuhamasisha shughuli za maendeleo,uzalishaji mali,kusimamia mapato,kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia,kuzuia migogoro ya ardhi,kutunza mazingira na kusimamia usafi.

Maelekezo mengine ni kuhamasisha wananchi wajiunge na Bima ya Afya,kutumia vyandarua,na kwamba mwakani 2025 wasimamie zoezi la watoto kwenda shule madarasa ya awali,la kwanza na kidato cha kwanza, pamoja na kutowaficha watoto wenye ulemavu bali wawapatie haki yao ya elimu.
Katika hatua nyingine,amewasisitiza viongozi wa Serikali za Mitaa kutoka CCM,kwamba washirikiane na wapinzani katika kusikiliza mawazo yao, na kufanya kazi kwa pamoja ili kusukuma gurudumu la maendeleo.

Naoa baadhi ya viongozi hao akiwamo Mwenyekiti wa kitongoji cha Kasubuya kutoka CHADEMA Juma Tungu, amesema mafunzo ambayo wamepatiwa yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao katika kuwatumikia wananchi.
Naye Afisa uchaguzi kutoka Halmashuri ya wilaya ya Shinyanga Oscar Lupavila,ametaja takwimu kwamba wenyeviti wa vijiji katika Halmashuri hiyo wapo 126 na vitongoji 856.

Aidha mafunzo waliyopewa viongozi hao, ni sheria za uendeshaji wa Mamlaka wa serikali za mitaa,muundo, majukumu,madaraka ya vijiji,mitaa, na vitongoji, utawala bora,maadili,uendeshaji wa vikao na mikutano.
Mafunzo mengine ni usimamizi wa miradi shirikishi ya kijamii na usimamizi wa fedha katika mamlaka za serikali za mitaa.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye mafunzo ya uongozi kwa wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Naye Afisa uchaguzi kutoka Halmashuri ya wilaya ya Shinyanga Osca Lupavila akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Wawezaji wa Mafunzo.
Viuongozi wa Vitoji walioshinda kuchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27,2024 kupitia CHADEMA.
Mafunzo ya uongozi kwa wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga yakiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464