SHUWASA KUTUMIA MILIONI 338 KUPANUA MTAMBO WA KUCHAKATA TOPE KINYESI
MAMLAKA ya Majisafi na usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA),wapo kwenye utekelezaji wa kupanua mtambo wa kuchakata tope kinyesi.
Mtambo huo wa kuchakata tope kinyesi upo kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga.
Meneja uendeshaji miundombinu kutoka SHUWASA Mhandisi Wilfred Lameck, akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la upanuzi wa mradi huo, amesema lengo ni kuongeza utoaji wa huduma kwa kukidhi mahitaji ya wananchi.
Amesema awali mtambo huo wa kuchakata tope kinyesi,ulikuwa na uwezo wa kuchakata Mita za ujazo 40, na sasa wanaongeza Mita 60 ili kufika Mita 100.
"Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 62, na gharama zake ni shilingi milioni 338," amesema Mhandisi Lameck.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola, amesema mtambo huo wa kuchakata tope kinyesi, awali waliubuni na kutekelezwa kwa kushirikiana na shirika la maendeleo la uholanzi (SNV),pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Amesema mtambo huo, ni wakuchakata tope kinyesi kutoka majumbani pekee na utanufaisha wananchi laki mbili wa manispaa ya Shinyanga na miji jirani.
Aidha,amemuagiza Mkandarasi ambaye anatekeleza mradi huo, kwamba aukamilishe kwa wakati na kiwango kinachotakiwa kwa kuonekana thamani ya fedha.
Kwa upande wake Mkandarasi Swalehe Maganga kutoka Kampuni ya Kanuta Engineering Supply, amesema mradi huo ataukamilisha ndani ya muda wa mkataba.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola akizungumzia upanuzi wa Mtambo wa kuchakata Tope Kinyesi.
Meneja uendeshaji miundombinu kutoka SHUWASA Mhandisi Wilfred Lameck akizungumzia upanuzi wa mtambo wa kuchakata Tope Kinyesi.
Mkandarasi Swalehe Maganga kutoka Kampuni ya Kanuta Engineering supply, akizungumzia utekelezaji wa mradi huo.
Mafunzi wakiendelea na ujenzi.
Gari likimwaga Majitaka kwenye Mtambo huo wa kuchakata Tope Kinyesi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464