Rais Samia atoa zawadi ya chakula kwa watoto wenye mahitaji maalumu kituo cha Buhangija Shinyanga kufurahia sikukuu za mwisho wa mwaka
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa zawadi ya chakula na vitu mbalimbali kwa watoto wenye mahitaji maalumu, ambao wanalelewa kituo cha Buhangija Manispaa ya Shinyanga, kwa ajili ya kufurahia sikukuu za mwisho wa mwaka.
Zawadi hizo zimetolewa leo Desemba 28,2024,na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Anamringi Macha.
Mtatiro amesema, Rais Samia ana moyo wa upendo,na kwamba kila mwaka amekuwa akitoa zawadi ya chakula kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu, ili kufurahia sikukuu za mwisho wa mwaka.
"Shughuli ya leo ni kufikisha zawadi za mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa watoto hawa wenye mahitaji maalumu hapa Buhangija, ili wafurahie sikukuu za mwisho wa mwaka,"amesema Mtatiro.
"Matendo haya ambayo anafanya Rais ni matendo ya kipekee, hivyo tunapaswa kuyaenzi na kuyatekeleza, na zawadi hizi ametoa katika maeneo mbalimbali kwa kuwakumbuka watoto wenye uhitaji," ameongeza.
Aidha,amesema Rais Samia siyo tu ametia zawadi hizi pekee kwa watoto hao wenye mahitaji maalumu,bali amekuwa akiboresha miundombinu rafiki kwao,ikiwamo ujenzi wa mabweni pamoja na kuwaletea wataalamu wakiwamo walimu wenye taaluma maalumu.
Ametoa wito pia kwa watoto hao,kwamba waendelee kusoma kwa bidii ili watimize ndoto zao na wasijione wanyonge, sababu serikali ipo pamoja nao chini ya Dk.Rais Samia Suluhu Hassan.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Charles Luchagula, ametaja zawadi ambazo zimetolewa na Rais Samia, kuwa ni mchele kilo 100,ngano kilo 50,unga wa sembe kilo 50,sukari kilo 50, na mafuta lita 20.
Zawadi zingine ni taulo za kike,mafuta ya kupaka,chumvi,juice,nyanya pamoja na mbuzi beberu.
Nao baadhi ya watoto hao wenye mahitaji maalumu,wamemshukuru Rais Samia, kwa kuwapatia zawadi hizo za chakula,kwa ajili ya kufurahia sikukuu za mwisho wa mwaka.
Mwalimu wa shule ya msingi Buhangija Jumuishi Fatuma Jilala, ambaye ndiye mlezi mkuu wa kituo hicho,amesema kuna wanafunzi wenye mahitaji maalumu 146, huku akimpongeza Rais Samia, kwa kutatua changamoto mbalimbali shule hapo, ikiwamo ujenzi wa mabweni,kutoa fedha ya chakula kila mwezi,upatikanaji wa vifaa maalumu na vitabu vya watoto wenye mahitaji.