RC MACHA AKEMEA MAISHA YA “SINGLE MOTHER” ALIPONGEZA SHIRIKA LA FHI360 KUENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA VVU


RC MACHA AKEMEA MAISHA YA “SINGLE MOTHER”

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amekemea tabia ya baadhi ya wanawake kupenda kuishi maisha ya bila wanaume na kulea watoto peke yao, huku mtoto akiwa hamjui Baba yake “Single Mother” na kwamba huo ni moja ya ukatili na hawawezi kufanikiwa kimaisha.
Amebainisha hayo leo Desemba 18,2024 wakati Shirika la FHI 360 kupitia mradi wa EPIC,lilipokuwa likikabidhi vifaa vya kujikwamua kiuchumi kwa mabinti ambao ni wanufaika wa mradi huo, pamoja na kukabidhi kabati 15 za utunzaji file katika vituo vya afya kwenye halmashauri tatu za mkoa huo.

Mradi huo wa Epic,umelenga kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi (VVU), kwa mabinti wenye umri wa kuanzia miaka 15-24 ambao wapo nje ya shule.
Macha akizungumza kwenye hafla hiyo, amesema ilikukabiliana na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi, ni vyema watu wakawa na mpenzi mmoja na kuishi kwa uaminifu, kuliko kupenda kuonja onja kila mahali,huku akikemea tabia ya baadhi ya wanawake ambao wanapenda kuwa na mahusiano na wanaume mbalimbali,na kuzaa watoto na kuishi bila wanaume na kujiita “Single Mother”

“kuishi maisha ya Single Mother ni moja ya kuwafanyia ukatili watoto, huwezi kuishi na mtoto ambaye hamjui Baba yake, huo ni ukatili, na pia kuishi maisha hayo huwezi kutoboa kimaisha bali utaishi maisha ya tabu ya kuonja onja kwa wanaume hovyo, mwisho wa siku una ambulia virusi vya ukimwi,”amesema Macha.
Ameongeza kuwa, kuna mwanamke mmoja ambaye anaishi maisha ya “Single Mother” alimpigia simu kumuona msaada, na kumwambia maisha yamemshinda, na kwamba ana watoto wanne na kila mtoto ana Baba yake, kitendo ambacho amewasihi wanawake wasipende kuishi maisha ya kuiga, bali watafute mwanaume mmoja na kuishi naye.

Pia, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo, kwamba wajenge utamaduni wa kupima afya zao pamoja na virusi vya ukimwi (VVU),ili wapate kujua afya zao na kujilinda zaidi, na kama wamepata maambukizi hayo, waanze kutumia dawa za kufubaza makali.
Amesema mtu ambaye amepata maambukizi ya virusi vya ukimwi, akitumia dawa vizuri hataweza tena kumwambukiza mtu mwingine pamoja na kuishi maisha marefu, na kwamba katika Mkoa wa Shinyanga watu elfu 72 wanatumia dawa za kufubaza makali.

Ametaja takwimu za maambukizi ya virusi vya ukimwi mkoani Shinyanga, kwamba yapo juu asilimia 5.6 huku hali ya maambukizi ya kitaifa ni asilimia 5.1.
Aidha, amelipongeza shirika la FHI360, katika kuendelea kushirikiana na Serikali dhidi ya mapambano ya virusi vya ukimwi (VVU), na kuwasaidia mabinti hao vitendea kazi ambavyo vitawakwamua kiuchumi, na kuondokana na tamaa za dunia.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu, amesema hafla hiyo ni mwendelezo wa shughuli za wadau wao katika mapambano dhidi ya virusi vya ukimwi, na kwamba walianza na utoaji wa elimu kwa mabinti kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, na sasa wanawapatia vitendea kazi ili wajikwamue kiuchumi.
Amesema kundi kubwa ambalo linapata maambukizi mapya ya VVU ni wasichana kuanzia umri miaka 15-24, na kwamba tafiti zilifanyika na kuonekana tatizo kubwa la mabinti hao, ni kukabiliwa na maisha duni,ukosefu wa elimu, pamoja na kuwa na tamaa za maisha ya dunia, na kujiingiza kwenye vitendo vya ngono.

Naye Kaimu Meneja wa Mradi wa EPIC Getrude Saleko kutoka shirika la FHI 360, Amesema mradi huo ulianza mwaka 2020, kwa lengo la kuzuia maambukizi mpya ya virusi vya ukimwi (VVU), kwa Mabinti wenye umri wa kuanzia miaka 15-24 ambao wapo nje ya shule, na kuwapatia elimu ya mabadiliko ya tabia, Afya ya uzazi na mpango,elimu ya kiuchumi ili wasijiingize kwenye mazingira hatarishi.
Amesema mwaka 2021 walifungua Karakana 16 mkoani Shinyanga, na kwamba Manispaa ya Shinyanga zipo mbili katika Kata ya Mwawaza na Ibadakuli, na kuwapatia Mabinti cherehani kwa ajili ya kujifunza kushona, ili wapate ujuzi wa kujikwamua kiuchumi.

Ameongeza kuwa, leo wamewapatia Mabinti hao vyerehani,majora,vifaa vya saloon,computer na printer mashine, vifaa ambavyo watajifunza na kupata ujuzi ambao watautumia kujiajiri na kuendesha maisha yao,na kuondoka kuishi katika maisha hatarishi.
Nao baadhi ya Mabinti ambao ni wanufaika wa mradi huo wa EPIC kutoka shirika la FHI 360, akiwamo Mbuke Mipawa, amepongeza shirika hilo kwa kuwatoa kuishi katika maisha hatarishi, ili kuepukana kupata maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi, na kwamba sasa hivi wamepata ujuzi ambao wataendesha maisha yao.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwneye hafla hiyo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu akizungumza kwenye hafla hiyo.
Kaimu Meneja wa mradi wa EPIC Getrude Saleko akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mnufaika wa mradi wa EPIC Mbuke Mipawa, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Kaimu Meneja wa mradi wa EPIC Getrude Saleko, (kushoto)akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, vifaa hivyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha (kulia)akimkabidhi Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga vifaa hivyo.
Muonekano wa baadhi ya vifaa.
Wanufaika wa mradi wa EPIC kutoka Shirika la FHI360.
Picha za pamoja zikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464