Na Sumai Salum, Kishapu
Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki mwa Ziwa Victoria Usharika wa Hosiana limeandaa bonanza la michezo lililopewa jina la Funga Mwaka na Yesu, ambalo limefanyika Disemba 31, 2024, katika viwanja vya michezo vya Shule ya Msingi Mhunze, Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga.
Bonanza hilo limehusisha timu ya KKKT FC na Bodaboda FC, ambapo Bodaboda FC wameshinda kwa mabao 4-1.
Akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Wilaya, Fatma Mohamed, Mchungaji wa KKKT, Patric Zengo, amesema kuwa lengo la bonanza hili ni kufunga mwaka kwa kumshukuru Yesu na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa upandaji miti ya matunda kwa ajili ya kuboresha afya.
"Ndugu mgeni rasmi, na Katibu Tawala wetu, mliokuja na Afisa Tawala Bwana Fadhiri, tunawashukuru sana kwa upendo wenu kwani mmetuheshimu. Tumeamua kufanya hili kanisa la Kiinjili ili kuwahamasisha vijana wetu kufunga mwaka na Yesu. Pia, tutagawa miti 50 ya matunda ili kuboresha mazingira yetu," amesema Mchungaji Zengo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Fatma Mohamed, amepongeza uongozi wa kanisa kwa ubunifu wao na kusema michezo imeleta matumaini na umoja kwa wananchi wa Kishapu.
Amesisitiza kuwa michezo ni njia nzuri ya kuleta upendo na mshikamano katika jamii.
“Kwa kweli Funga Mwaka na Yesu ni bonanza nzuri sana. Nimeona wachezaji wengi walikuwa wakishiriki michezo katika mabonanza mbalimbali, na hii ni kwa sababu ya umoja na upendo uliopatikana kupitia michezo. Pia tunayo mazoezi kila Jumamosi ambayo ni kwa faida ya afya zetu. Hongera kwa mchungaji kwa kuhamasisha upandaji miti ya matunda, leo nimejionea mwenyewe na kuthibitisha," amesema Fatma Mohamed.
Katika mchezo wa mpira wa miguu, magoli yote yamefungwa katika kipindi cha pili. Wafungaji wa Bodaboda FC walikuwa Sangalali Nenga (alifunga magoli matatu), Baraka Lisu (alifunga moja), na Shabani Khamis (alifunga moja), wakati mfungaji pekee wa KKKT FC alikuwa Richard Mwashambwa.
Aidha, miti ya matunda iliyogawiwa kwa wananchi ilijumuisha mipapai, machungwa, mapera, na makakala (passion fruit).
Mgeni rasmi pamoja na mchungaji kiongozi wamesisitiza umuhimu wa kuitunza miti hiyo kwa manufaa ya afya ya jamii, kwa kuzingatia kauli mbiu ya kanisa la "Mti Wangu, Nchi Yangu, Mazingira Yangu".
Baada ya bonanza, wachezaji wa timu zote mbili pamoja na mgeni rasmi wameshiriki chakula na vinywaji kwa pamoja katika ukumbi wa kanisa la KKKT Hosiana Mhunze, ikiwa ni ishara ya mshikamano na furaha ya kufunga mwaka kwa umoja.