Na Mwandishi Wetu, JAB, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema, kazi ya Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) ni kulea na kusimamia maadili ya waandishi wa habari na siyo vinginevyo.
Prof. Kabudi amesema hayo Jumatano Desemba 18, 2024 jijini Dar es Salaam, wakati alipokutana na wadau, Waandishi wa Habari na baadhi ya Watumishi wa Idara ya Habari Maelezo ili kutambuana baada ya kuteuliwa kuongoza wizara hiyo hivi karibuni.
Prof. Kabudi amesema, JAB imekuja kama mtumbwi wa kuwapitisha waandishi wa habari kwenye bahari yenye mawimbi mengi na kuwafikisha katika bandari salama ya kuwa na waandishi wenye weledi, wanaozingatia maadili yao na wanaotoa mchango wao katika taifa.
Amesema, ameshaongea na Katibu Mkuu wa wizara hiyo (Bw. Gerson Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali) na kumweleza kuwa miongoni mwa watu atakaokaa nao kwa muda mrefu ni Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) na kwamba kufanya hivyo ni kuondoa taswira kuwa bodi hiyo imekuja kuwa rungu.
Prof. Kabudi amesema, kuteuliwa kwa Bodi ya Ithibati ni mafanikio mengine ya Serikali ya Awamu ya Sita, na lengo ni kuendelea kulinda maadili ya waandishi wa habari, kama ilivyo katika Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, sura Na. 229.
Aidha, amewaambia wadau hao wa habari kwamba uzinduzi rasmi wa bodi hiyo utafanyika mwezi Januari 2025, na watajulishwa kabla ya uzinduzi huo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464