Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya leo imeteketeza kilogramu 614.12 za dawa za kulevya katika kiwanda cha saruji cha Twiga, kilichopo Wazo, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika tukio hilo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo alisema kuwa, kati ya dawa zilizoteketezwa, kilogramu 601.87 ni methamphetamine na kilogramu 12.25 ni heroin ambapo dawa hizo zilikuwa zinashikiliwa kama vielelezo, na mahakama za Hakimu Mkazi Kibaha na Kisutu ziliamuru uteketezaji wake kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo wakati kesi husika bado zinaendelea.
"Uteketezaji wa dawa hizi unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015 pamoja na kanuni zake. Sheria hii inaruhusu uteketezaji wa dawa hizi kufanyika kabla, wakati, au baada ya shauri kumalizika mahakamani," alieleza Kamishna Lyimo.
Kamishna alifafanua kuwa uteketezaji huo unafanywa kwa njia zinazozingatia usalama wa afya ya watu na utunzaji wa mazingira, huku ukisimamiwa na wadau mbalimbali waliotajwa kisheria.
Aidha, Kamishna Lyimo alibainisha kuwa katika mwezi huu wa Desemba pekee, mamlaka imefanikiwa kuteketeza ekari 12 za mashamba ya bangi katika mkoa wa Tabora, pamoja na kilogramu 398.105 za dawa mbalimbali mkoani Mtwara. Pia, mamlaka inatarajia kuteketeza kilo 126.21 za mirungi mkoani Arusha katika siku chache zijazo.
Kamishna aliwapongeza wadau wote waliofanikisha uteketezaji wa dawa hizo na kuendelea kushirikiana na mamlaka katika juhudi za kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya. Alihitimisha kwa kusema kuwa zoezi la uteketezaji litaendelea nchi nzima, kadri mahakama zitakavyoendelea kutoa amri.
"Tunaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa dawa hizi haramu zinadhibitiwa kwa ustawi wa jamii yetu," aliongeza.