MWEKEZAJI BINAFSI AIOMBA SERIKALI KUJENGA UWANJA WA NDEGE MANYARA

Mwekezaji Mzawa kutoka Mkoani Manyara.

Na Jaliwason Jasson, Babati 

MWEKEZAJI mzawa  wa mkoani Manyara David Mulokozi amewashangaza wananchi wa Babati kutua na Helkopita yake binafsi ambayo amenunua ili kurahisisha usafiri katika kufanya shughuli zake huku akiiomba serikali kujenga uwanja wa ndege Manyara au kumruhusu ajenge yeye halafu serikali ije imlipe ili kurahisisha usafiri wa anga.

Mulokozi ametua leo Desemba 18 katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa akiwa na familia yake akitokea ughaibuni.

Aidha amesema gharama inayotumiwa na wananchi kufuata uwanja wa ndege wa Kilimanjaro(KIA) na uwanja wa ndege wa Dodoma ni kubwa ambapo fedha inayotumika kwenye magari kufuata viwanja vya ndege ili kusafiri inatosha kulipia usafiri wa ndege kwenda Dar es salaam.

Bilinea huyo amesema wakati anafatilia vibali vya kununua ndege hiyo hajapata usumbufu kwa kuwa alifuata kila hatua iliyotakiwa.

"Naomba serikali itujengee uwanja wa ndege Manyara ili kurahisisha usafiri na kama ikiniruhusu kujenga mimi mwenyewe niko tayari hata kesho maana huu ni uwekezaji,"amesema Mulokozi

Vile vile ameeleza kuwa ndege hiyo itasaidia kurahisisha biashara zake za kiwanda cha Mati Super Brands Limited ambapo ataweza kusafiri mikoa saba mpaka 10 kuongea na wateja wao.

Amesema amefungua njia kwa wafanyabiashara wengine wa Manyara wenye uwezo anasema wanunue ili kuongeza wigo wa usafiri wa anga na ndio uwekezaji wenyewe.

Mfanyabiashara huyo amesema baada ya kutoka Babati ndege hiyo inaelekea Bukoba mkoani Kagera itapita Mwanza kuweka mafuta na kwenda Bukoba halafu itarudi Babati  na baadaye itaenda kupaki Arusha au KIA.

Naye mkazi wa Babati Inyasi Melicholi alimpongeza Mulokozi kwa uthubutu na kusema ameiheshimisha Babati na mkoa wa Manyara.






Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464