TRA SHINYANGA YAHIMIZA WAFANYABIASHARA KULIPA KODI KABLA YA DESEMBA 30,2024

 

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Josephat Mwaipaja akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Desemba 03,2024

Na mwandishi wetu – Malunde 1 blog

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imewahimiza Walipa Kodi wote kulipa kodi walizokadiriwa pamoja na malimbikizo yote kabla ya Desemba 30,2024 ili kuepuka riba baada ya kipindi hicho.

Rai hiyo imetolewa leo Jumanne Desemba 3,2024 na Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Josephat Mwaipaja wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu Uwasilishwaji wa Ritani na Malipo ya Kodi ya Mapato awamu ya nne.


“Mwezi Desemba ni mwezi muhimu katika makusanyo ya kodi kwani ni mwezi wa malipo ya kodi kwa awamu ya nne kwa mwaka huu wa 2024/2025. Ni kipindi ambacho kodi nyingi zinapaswa kulipwa, hivyo nichukue nafasi hii kuwahimiza wafanyabiashara wote kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya awamu ya nne pamoja na malimbikizo yote ya kodi wanayodaiwa kabla ya tarehe 30.12.2024”,amesema Mwaipaja.

Katika hatua nyingine amewataka wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za biashara ili kupata makadirio sahihi ya kodi na kupunguza malalamiko ya makadirio ya kodi.

“Tunaendelea kuwakumbusha walipakodi kuhakikisha wanatoa risiti za EFD wanapouza bidhaa au huduma na pia wanunuzi wa bidhaa au huduma wahakikishe wanadai risiti zenye thamani sawa na pesa waliyotoa wakati wa kununua bidhaa au huduma”,ameeleza Mwaipaja.
Aidha Mwaipaja amesema TRA imetenga siku ya Alhamisi kwa ajili ya kuwasikiliza walipa kodi ili kupokea kero,malalamiko na maoni mbalimbali.

Kodi huipatia uwezo serikali kutekeleza miradi iliyopangwa kwa ajili ya wananchi kama vile shule,hospitali, huduma za kiuchumi, umeme, barabara, huduma za ulinzi na usalama na huduma za kiutawala.

Ukadiriaji wa kodi ni shughuli inayofanya mlipakodi kufahamu kiasi cha kodi kulingana na kumbukumbu za mlipakodi zilizopo ambapo Malipo ya kodi yalikadiriwa hufanyika kwa awamu nne (Machi, Juni, Septemba, Desemba).

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464