WADAU WA UTALII KANYIGO KUU WAHIMIZWA KUTUMIA FURSA ZILIZOPO MAENEO YAO KATIKA KUBORESHA MAISHA YAO KIUCHUMI
Baadhi ya watalii ndani ya ziwa Victoria wakielekea kutembelea pango kanisa Nyangambo
Pango lililotumika kama kanisa.
Na Mutayoba Arbogast, Bukoba
WANANCHI wazawa wa Kata za Kanyigo na Kashenye (Kanyigo kuu) wilayani Missenyi, waishio maeneo mahalia na nje wakiwemo wageni, wameitumia fursa ya likizo ya sikukuu za mwisho na mwanzo wa mwaka kujumuika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ukiwemo utalii wa ndani.
Wananchi hao wakiongozwa na dhima, 'Entabuko' yaani 'Asili yangu' kwa lengo la kujua, kuhifadhi na kurithisha kwa vizazi vijavyo historia, utamaduni, mila na tunu za Kanyigo kuu, wametembelea maeneo mbalimvali ya kihistoria, ziara iliyowashirikisha pia wanafunzi wawakilishi wa shule za msingi na sekondari katika kata hizo mbili, wawakilishi wa serikali za vijiji, viongozi wa dini nk.
Dk. Daniel Ndagala ambaye ndiye mwandaaji wa ziara hii pia
mwanzilishi na mkurugenzi wa Nyumba ya makumbusho Kanyigo (Kanyigo museum), mdau wa utalii na utamaduni anasema,
"Lengo la ziara hii ya Entabuko ni kuwawezeha watu wa Kanyigo kuu, ikiwemo sehemu ya Nyangoma (Nangoma-Uganda) kutambua na kufahamu fursa na changamoto zilizomo, na kufahamu mambo mbalimbali yatakayosaidia kuboresha maisha yao".
Watalii ndani ya ziwa Victoria kutembelea pangokanisa Nyangambo( picha A.Mutayoba)
Kwenye pango hilo kulianzishwa kanisa (pango kanisa) ambamo Wakristo Waprotestanti wa mwazo waliendesha ibada zao miaka ya mwanzo ya Ukristo katika Buhaya (Bukoba) wakiwa mafichoni wakihofia maisha yao mnamo 1896, miongoni mwa wahubiri wa mwanzo wa injili wakiwa ni Zacharia Itake, Ibrahim Mpanda Kyaro na Isaya Kibira.
Pia watalii hao walijionea na kufurahia mkondo wa maji wa mto Kagera unavyokata maji kuingia katika ziwa Victoria kuelekea Kakazini yaani mto Naili.
Kwenye hitimisho la ziara hiyo iliyofanyika viwanja vya nyumba ya makumbusho Kanyigo (Kanyigo museum), kulifanyika shughuli mbalimbali za kiutadamaduni zikiwemo usimuliaji hadithi ( storytelling), kutega na kutegua vitendawili nk
Baadhi ya wazee watalii wa ndani wakiongozwa na mwandaaji Mkuu wa Entabuko Dk .Daniel Ndagala (mwenye Tshirt ya bluu)
Mashujaa wa maendeleo Kanyigo Kuu watambuliwa rasmi na 'Entabuko'
Jukwaa hilo la Asili yangu, baada ya mchakato wa kuwatambua watu waliotoa/ wanaotoa mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya Kanyigo kuu, limewatambua rasmi watu hao, na zoezi hilo litakuea endelevu kutokana na mapendekezo ya wananchi juu ya akina nani wanaostahili heshima hiyo.
Mwaka huu 2024, mashujaa hao waliotambuliwa ni Stepano Luwago(1994-1978) wa kijiji Kigarama ambaye alikuwa fundi mwashi na seremala,mnamo mwaka 1936 alibuni na kutengeneza mashini za miti za kukoboa kahawa na kusaga nafaka, ambaxo zilirahisisha kazi na kuchochea kazi ya kuinua uchumi, Frederick Rwegarulila (1928-1978) aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa wizara ya maji ambaye alisimamia vizuri progamu ya usambazaji wa maji safi na salama nchini, ikiwemo Kanyigo kuu, pia mwanzilishi wa Chuo cha maji kilichobeva jina lake.
Wengine waliotambuliwa ni Samweli Mutatina Kassano (1929-1997) aliyejijengea umaarufu mkubwa katika siasa, kiongozi wa Jumuiya ya wazazi( TAPA), akisimamia pia ujenzi wa shule za msingi Kanyigo na Nshumba.
Kanali (mstaafu) Ngemela Eslom Lubinga, ametambuliwa kwa uchapakazi, nidhamu, unadhifu na unyenyekevu, mambo ambayo yanachochea vijana wengi kupenda kujiunga na jeshi.
Aidha wametambuliwa viongozi waanzilishi wa shirika la maendeleo KADEA, lililoanzishwa mwaka 1984 ambayo inamiliki pia shule ya sekondari Kanyigo.
Jamii yapewa changamoto kutafiti vizazi vya babu zao
Mzee Enock Kamuzora, mdau wa maendeleo, mwalimu mstaafu na mwanahistoria mzaliwa wa kijiji Kigarama. ameishauri jamii kutafiti vizazi wa babu zao ili kujua mbari zao (lineage) kama yeye alivyofanya hadi kufikia kwa Mukama Igaba ll wa Bunyoro aliyetawala around 1500, yaani takriban miaka 600 iliyopita.
Mimi na wewe tunavijua vizazi vingapi? hebu vitaje kimoyomoyo!
Mzee Kamuzora anajigamba,"Naitwa Enock Kamuzora bin Augustine Lwehumbiza bin Kamuzora bin Lwabusimbi bin Kaija bin Luhanga bin Muraba bin Butolilo bin Luganyoile- olugundu bin Mpindi bin Munera bin Mbogo bin Ishamura Nyakabinga (Omukama wa Kiziba) bin Kibi Nyakìiru (Kibi l, Omukama wa Kiziba) bin Igaba ll (Omukama wa Bunyoro).