SERIKALI KUGAWA VYANDARUA VYENYE DAWA BURE KUTOKOMEZA UNGOJWA WA MALARIA
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEM, wameanzisha kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa bure kwa kila Kaya,ili kupambana na ugonjwa wa malaria.
Hayo yamebainishwa leo Januari 6,2025 na Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya Peter Gitanya kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria (NMCP),kwenye kikao kazi na waandishi wa habari wa mkoa wa shinyanga,juu ya kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa kwa wananchi.
Amesema serikali kupitia mpango wake wa kudhibiti malaria nchini,wameanzisha kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa bure kwa wananchi kwa kupita kila Kaya, ili kupambana na ugonjwa wa malaria na kuutokomeza kabisa ifikapo 2030.
“Mkoa wa Shinyanga vitasambazwa vyandarua vyenye dawa milioni 1.5 na Kaya zote zitafikiwa, na sasa tupo kwenye zoezi la uandikishaji kaya kwa kaya, na chandarua kimoja watapewa watu wawili wawili kwa kila Kaya,”amesema Gitanya.
Amesisitiza kwamba, kwa Kaya ambayo haitaandikishwa haitaweza kupewa chandarua,na kuwasihi washiriki zoezi hilo kikamilifu, ambapo maafisa watakuwa wakipita kwenye Kaya zao kuchukua taarifa, pamoja na kuwapatia kadi maalumu kwa ajili ya kuja kupewa chandarua.
Amesema kwamba zoezi la uandikishaji lilishaanza tangu januari 2 na litakwenda hadi januari 15, na tarehe 16 zoezi rasmi la usambazaji vyandarua litaanza na kuzifikia Kaya zote ambazo zimeandikishwa.
Aidha, akizungumzia hali ya malaria nchini, ameutaja mkoa wa shinyanga kwamba unashika nafasi ya 4 kitaifa, kuwa na kiwango cha juu cha malaria asilimia 16, ambapo kitaifa ni asilimia 8, huku Tabora ikishika nafasi ya kwanza asilimia 24, ya Pili Mtwara asilimia 20, na ya tatu ni Kagera asilimia 18.
Naye Happines Nania kutoka Wizara ya Afya, amesema kwa mwananchi ambaye atapoteza kadi ambayo alipewa wakati akiandikishwa kwa ajili ya kupewa chandarua, anapaswa kwenda kwenye kituo husika ili apewa chandarua chake sababu taarifa zake zitakuwepo,huku akisisitiza pia utunzaji wa vyandarua hivyo na kuvitumia kwa matumizi sahihi yaliyokusudiwa.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu, awali akizungumza wakati akifungua kikao hicho,ameipongeza serikali kwa kampeni hiyo ya mapambano dhidi ya malaria,na kuwasihi waandishi wa habari kupitia kikao kazi hicho,watumia kalamu zao kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya vyandarua vyenye dawa.
Amewasisitiza pia waandishi wa habari kuondoa upotoshaji ambao umekuwa ukienezwa juu ya matumizi ya vyandarua hivyo vyenye dawa, na kusababisha baadhi yao kutovitumia, na kueleza kwamba vyandarua hivyo ni salama na havina madhara yoyote.
“Waandishi wa habari tumieni kalamu zenu kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya vyandarua vyenye dawa, ili tuijenge Shinyanga isiyo na Malaria,”amesema Mlyutu.
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru,akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari mkoani humo,ameipongeza serikali kwa kuwashirikisha kwenye kampeni hiyo,ambapo watatumia kalamu zao kupeleka ujumbe sahihi kwa wananchi, juu matumizi sahihi vya vyandarua vyenye dawa na kukabiliana na ugonjwa wa Malaria.
TAZAMA PICHA👇👇
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Afisa kutoka TAMISEM Best Yoram akizunguma kwenye kikao kazi hicho.
Afisa mradiwa Malaria kutoka Wizara ya Afya Willfred Mwafongo akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Mwakilishi wa wajamii Gesonko Paul akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Mratibu wa Malaria Mkoa wa Shinyanga Betty Shayo akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya Peter Gitanya kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria (NMCP)akiwasilisha mada kwenye kikao kazi hicho.
Afisa kutoka Wizara ya Afya Atley Kuni akiwasilisha mada kwenye kikao kazi hicho.
Afisa kutoka Wizara ya Afya Happines Nania akiwasilisha mada.
Mratibu wa elimu ya afya kwa umma Mkoa wa Shinyanga Moses Mwita akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Kikao kazi kikiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464