RC MACHA ATOA MAAGIZO MAZITO KIKAO KAZI NA WATUMISHI WA SERIKALI AKITOA SALAMU ZA MWAKA MPYA 2025

RC MACHA ATOA MAAGIZO MAZITO KIKAO KAZI NA WATUMISHI WA SERIKALI AKITOA SALAMU ZA MWAKA MPYA 2025

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amefanya kikao kazi na Watumishi wa Serikali na wakuu wa Taasisi za Serikali mkoani humo,kwa kuwapatia maagizo ya utendaji kazi,pamoja na kutoa salamu za mwaka mpya 2025.
RC MACHA

Amefanya kikao kazi hicho leo Januari 9,2025 katika ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkoa.

Amesema tangu ateuliwe na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,ameshafikisha miezi 9,huku akiwashukuru Watumishi wa Serikali kwa kumpatia ushirikiano katika kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi na kumwakilisha vyema Rais Samia.
RAS CP Salum Hamduni

“Kikao hiki ni cha utendaji na kutoa salamu za mwaka mpya 2025 na tunamshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka 2024 tukiwa salama,na tunampongeza Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi katika mwaka uliopita mkoani kwetu zaidi ya Trilioni Moja, na zimetekeleza miradi mingi ya maendeleo,”amesema Macha

Amesema katika mwaka huu wa 2025, amewasihi Watumishi wa Serikali waendelee kufanya kazi kwa kujitolea,kutanguliza uzalendo,kushirikiana na kuwatumikia wananchi kwa moyo wote ikiwamo kutatua changamoto zao,na siyo kufanya kazi kwa kujionyesha na kuposti mitandaoni.
Aidha, amesema pamoja na salamu hizo za mwaka mpya 2025, ni vyema wakakumbushana mambo ya kufanya kwa kuanza mwaka mpya.

ELIMU

Katika suala la elimu,amesema kwamba shule zote zinafunguliwa Januari 13, na kwamba Wakurugenzi na Maafisa elimu wanapaswa kuhakikisha watoto wote ambao wanasifa ya kuanza elimu ya awali na msingi wanaandikishwa bila ya vikwazo vyovyote na kuanza masomo,pamoja na wale wa kidato cha kwanza wanajiunga na shule walizochaguliwa.
Amewasihi wazazi, kwamba licha ya elimu kutolewa bure nao wanapaswa kuwajibika kwa watoto wao,na kuwatimizia mahitaji yote ya shule,huku akiwaonya kutowaficha ndani watoto wao wenye ulemavu, bali wawapatie haki yao ya kielimu na kwamba watakaobainika serikali itawachukulia hatua kali.

Amesisitiza pia wazazi wasiwapeleke watoto wao kwenye shule binafsi kama fashioni ambazo zinagharama kubwa,na wakati hata shule za serikali zinafanya vizuri kitaaluma, na kwamba baadhi ya wazazi wamekuwa wakishindwa kuwalipa Ada watoto na kuwarudisha tena shule za serikali na kuwayumbisha.

MIGOGORO YA ARDHI

Amesema tatizo la migogoro ya ardhi mkoani humo limekuwa likisababishwa na pande mbili, ambao ni wananchi wenyewe pamoja na baadhi ya Watumishi wa serikali ambao siyo waaminifu kutoka Halmashauri na Idara ya Ardhi, ambapo ametoa onyo kali kwa watumishi ambao wamekuwa chanzo cha kuendeleza migogoro hiyo.
Ameagiza pia Halmashauri,TANESCO na Mamlaka za Maji, kuacha tabia ya kupelekea huduma, kwa watu ambao wamevamia maeneo na kujenga nyumba, bila ya kujiridhisha uhalali wao wa makazi kwa kupata nyaraka kutoka Idara ya Ardhi.

KILIMO

Amewaagiza Maafisa Ugani mkoani humo,kusimamia suala la kilimo, ili kuhakikisha Wakulima wanafanya kilimo chenye Tija na kupata mavuno mengi, na kwamba Serikali imeshawapatia vitendea kazi vyote.
AFYA

Amesema katika Hospitali zote za Halmashauri za mkoani humo zina Madaktari Bingwa pamoja na vituo vya Afya kuwa na vitendea kazi vya kutosha, na kwamba kinachotakiwa kwa Watumishi wa Afya ni kutoa huduma bora kwa wananchi, pamoja na kuwapatia elimu ya kukata bima ya Afya.

Ameagiza pia katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga na za Halmashuri zote, kuweka watu ambao watakuwa wamevaa Koti za “Niulize”kuanzia mwezi Februari ili kusaidia wagonjwa kupata huduma kwa urahisi.
MAZINGIRA

Ameagiza ufanyike usafi wa utunzaji wa mazingira kila mahali, kujenga vyoo na kuvitumia ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu,huku akisisitiza pia zoezi la upandaji miti kwa kila Halmashauri.

USTAWI WA JAMII

Amesisitiza kuendeleza mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia,huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa zawadi ya chakula kwa ajili ya sikukuu kwa makundi yenye uhitaji mkoani humo katika Halmashauri zote sita.
MAENDELEO YA JAMII

Amewataka Maaafisa Maendeleo ya jamii wawe makini na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 na kusiwepo na vikundi hewa,huku akiwasihi watu ambao wanaomba mikopo hiyo wabuni miradi mikubwa ya kuwainua kiuchumi.

MAJI

Amesisitiza pia utunzaji wa vyanzo vya maji, pamoja na Mamlaka husika kuongeza kasi ya usambazaji mitandao ya maji kwa wananchi.
TANESCO

Amewasihi katika uanganishaji wa huduma ya umeme kwa wananchi kwamba wazingatie kanuni na taratibu,huku akiipongeza Serikali kwa usambazaji kasi ya umeme, na kwamba kati ya vijiji 506 mkoani humo, vimebaki vijiji 7 tu ndiyo havina huduma hiyo.

TANROADS NA TARURA

Amewataka ma Meneja wake, kwa kwamba waendelee kusimamia Wakandarasi wafanye kazi zao kwa ufanisi na kuzikamilisha kwa wakati,pamoja na kushirikisha wananchi wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo ikiwamo na kuweka mabango kwa lugha ya Kiswahili.

USHIRIKA

Ameagiza wazisimamie vyema vyama vya msingi vya Ushirika AMCOS pamoja na kufanya ukaguzi wa vitabu vya fedha na kusimamia maslahi ya Wakulima.

BODI YA PAMBA

Wasimamie ubora wa mbegu za Pamba ambazo zinasambazwa kwa Wakulima,huku akionya wizi wa mbegu pamoja na madawa.

MAPATO

Ameziagiza Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato,kujenga mahusiano mazuri na wadau,kutozo Tozo zinazoendena na uwezo wa mfanyabiashara pamoja na kusiwepo urasmi wa kutoa Lessen.

MANUNUZI

Amewasihi Maafisa Manunuzi wazingatie Taaluma zao katika utendaji kazi pamoja kuzingatia bajeti na kuwalipa pia “Supply” madeni yao.

SAFARI ZA KUJIFUNZA

Amesema safari hizo ziendane na taratibu na zilete mafanikio, huku akitoa maelekezo kwa zile safari ambazo zimefanyika mwishoni mwa mwaka jana wampatie taarifa.

MBIO ZA MWENGE

Amesema Mbio za Mwenge za Mwaka jana Mkoa huo haukufanya vizuri, ambapo kati ya Mikoa 31 Shinyanga imeshika nafasi ya 19, na kwamba kwa mwaka huu 2025 zitafanyika mwezi Agost, na kusisitiza maandalizi yaanze kufanyika mapema, ili kushika nafasi ya juu.

MAVAZI OFISINI

Ametoa maekelezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo CP Salum Hamduni,kusimamia vyema suala la mavazi yenye maadili ofisini,huku akiwasihi Watumishi waendelee kufanya kazi kwa ushirikiano pamoja na kuwa na mahusiano mzuri.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464