WANANCHI SHINYANGA WAMEJITOKEZA KWA WINGI KUPATA MATIBABU YA MACHO BURE

WANANCHI SHINYANGA WAMEJITOKEZA KWA WINGI KUPATA MATIBABU YA MACHO BURE

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

WANANCHI wa Shinyanga,wamejitokeza kwa wingi kupata huduma ya matibabu bure ya macho,kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Macho wa Hospitali ya DrAgawals Tawi la Mwanza.
Zoezi hilo la utoaji wa matibabu bure ya macho,linafanyika leo Januari 10,2025 katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga Dk. Moshi Ryoba,akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo, amesema muitikio ni mkubwa wa wananchi kujitokeza kupata matibabu hayo ya macho.
“Tatizo la macho ni kubwa kwa wananchi wa Shinyanga,ukiangalia takwimu za watu ambao tumewaandikisha majira ya asubuhi tu, ni zaidi ya 250 na bado wanazidi kuja, hii inaonyesha wananchi wa hapa Shinyanga macho yanawasumbua sana,”amesema Dk.Ryoba.

Daktari Bingwa wa Macho Dk. Abubakari Mwatute,kutoka Hospitali ya Macho Dr.Agawals Tawi la Mwanza, amesema wanafarijika kuona wananchi wa Shinyanga, wameitikia kwa wingi kupata fursa ya matibabu bure ya macho,na kwamba kati ya watu 10 ambao wanawafanyia uchunguzi,Saba hadi Nane wanakabiliwa na tatizo la mtoto wa jicho.
Nao baadhi ya wananchi ambao wamejitokeza kupata matibabu hayo ya macho bure, akiwamo Charles Kisanga, wameishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau wa afya, na kuwapelekea madaktari bingwa wa macho na kuwapatia huduma bure, sababu wengine hawana uwezo wa kifedha.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464