WAFANYABIASHARA SHINYANGA WALIA UTITIRI WA KODI,WAKITOA MAPENDEKEZO KWA TUME YA RAIS YA MABORESHO YA KODI
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
WADAU wa kodi mkoani Shinyanga,wametoa mapendekezo yao namna ya kuboresha mifumo ya ulipaji kodi,kwa Tume ya Rais ya uboreshaji wa Kodi,huku wakipendekeza utitiri wa kodi uondolewe,hasa kwa taasisi mbili kutoza kodi ya aina moja,na utozwaji wa kodi ndani ya mtaji na siyo kwenye faida ambayo ni kodi ya ushuru wa huduma“Service Levy”.
Wametoa mapendekezo yao leo Januari 17,2025 kwenye Mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Lyakale Manispaa ya Shinyanga,huku mgeni Rasmi akiwa ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.
Awali akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda tume hiyo ya maboresho ya kodi,na kwamba dhamira yake ni kuinua uchumi wa nchi na kuwaletea maendeleo Watanzania.
Amesema taifa lolote duniani,kwamba ulipaji wa kodi ndiyo chanzo kikubwa cha mapato cha kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake na kuwaletea maendeleo wananchi,na kuwasihi Watanzania kumuunga mkono Rais Samia juu ya ulipaji kodi,na kutoa mapendekezo ya uboreshaji wa mifumo ya kodi, ili pande zote mbili zitapate kunufaika.
“Tafiti zinaonyesha miaka 50 ijayo, endapo tukiendelea kulipa kodi vizuri, nchi ya Tanzania itakuwa katika nchi 4 bora za Barani Afrika zenye uchumi mkubwa,”amesema Mtatiro.
Kaimu Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboreshaji ya Kodi Leonard Mususa, amesema Rais Samia aliunda Tume hiyo Oktoba 4 mwaka jana,kwa lengo la kuboresha mifumo ya ulipaji kodi, ili kuboresha ukusanyaji wa mapato pamoja na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.
Amesema tume hiyo imeundwa baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi juu ya utitiri wa kodi pamoja na tozo,na kwamba ulipaji wa kodi hapa nchini upo chini,ikilinganishwa na Afrika Jangwa wa Sahara.
“Umuhimu wa kodi ni kwa maendeleo ya nchi yetu,ndiyo maana Rais Samia anataka kupata mapendekezo ya uboreshaji wa mifumo ya kodi,ndiyo maana ametutuma tukusanye mapendekezo kwa nchi nzima,”amesema Mususa.
Mfanyabiashara wa sheli ya mafuta Mayengo Bageni kutoka wilayani Kahama, akitoa mapendekezo yake juu ya uboreshaji wa mifumo ya kodi,alilalamikia tatizo la utozwaji wa kodi ya ushuru wa huduma “Service Levy”kwamba ni tatizo kubwa kuwadidimiza kiuchumi wafanyabiashara sababu inatozwa kwenye mtaji na siyo sehemu ya faida kama kodi zingine.
Amesema tatizo jingine ni taasisi mbili kutoza kodi ya aina moja, na kutolea mfano kodi ya mabango ya barabarani ya kutangaza biashara zao, kwamba Halmashauri inatoza kodi na TANROADS nayo inatoza kodi.
“Mapendekezo yangu kwenye tume, hii kodi ya Service Levy iondolewe sababu inatozwa ndani ya mtaji, pia kuwepo na taasisi moja ambayo inatoza kodi na nyingine zibaki kutoa huduma,siyo kila taasisi kujiundia visheria na kuja kutoza kodi ya aina moja huku ni kuumiza wafanyabiashara,”amesema Mayengo.
Mfanyabiashara Gilitu Makula,naye alikazia suala la kodi ya “Service Levy”kwamba iondolewe sababu siyo rafiki kwao, kutokana na kutozwa ndani ya mtaji.
Katibu wa Chama cha Wachimbaji wadogo wa madini mkoani Shinyanga (SHIREMA)Gregory Kibusi,naye aliomba kuondolewa kwa utiriri wa kodi kwa wachimbaji hao, ili walipe kodi kihalali ili na wao wapate faida, na kusiwepo tena na tatizo la utoroshaji madini sababu ya kukwepa mlolongo wa ulipaji kodi.
Mwakilishi wa wakulima wadogo Kulwa Dotto,naye alitoa mapendekezo kuondolewe kwa tozo kwenye mazao ambayo yanatolewa mashambani kupelekwa nyumbani sababu hawaendi kufanya biashara bali ni kuyahifadhi kwanza.
Kaimu Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Shinyanga, Laurean Kyombo,alitoa mapendekezo juu ya kuondolewa kwa kodi kwenye malipo ya posho kwa watumishi wa sekta binafsi kama ilivyo kwa watumishi wa serikali, pamoja na kuondoa kodi kwenye zawadi za wafanyakazi bora ambazo huwepewa siku za Mei Mosi.
Ameomba pia kwenye mafao ya wastaafu ambayo wanapewa wasikatwe kodi.
Aidha,mapendekezo mengine yaliyotolewa kwenye mkutano huo ni kurudishwa kwa viparata vya wajasiriamali,kuondolewa kodi vifaa vya watu wenye ulemavu,na uagizaji mitambo ya madini.
TAZAMA PICHA 👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza kwenye mkutano huo.
Kaimu Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboreshaji ya Kodi Leonard Mususa akizungumza kwenye mkutano huo.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga David Lyamoga akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Katibu wa SHIREMA Gregory Kibusi akitoa mapendekezo kwenye mkutano huo.
Mfanyabiashara Gilitu Makula akitoa mapendekezo yake kwenye Mkutano huo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464