UTOLEWAJI ELIMU YA SHERIA UTATUMIKA UTARATIBU WA KUWAFUATA WANANCHI KATIKA MAENEO YAO MAADHIMISHO WIKI YA SHERIA NCHINI: JAJI MAHIMBALI

UTOLEWAJI ELIMU YA SHERIA UTATUMIKA UTARATIBU WA KUWAFUATA WANANCHI KATIKA MAENEO YAO MAADHIMISHO WIKI YA SHERIA NCHINI:JAJI MAHIMBALI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MAADHIMISHO ya wiki ya sheria katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga,yatazinduliwa rasmi januari 25 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,huku utoaji wa elimu ya sheria katika maadhimisho hayo utatumika utaratibu wa kuwafuata wananchi katika maeneo yao.
Hayo yamebainishwa leo Januari 20,2025 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali,wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Amesema siku ya sheria huashiria mwanzo wa kuanza kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka mpya husika baada ya kumalizika kwa likizo ya Mahakama inayoanza kila tarehe 15 Desemba na kumalizika januari 31 ya mwaka unaofuata,ili kuanza rasmi utendaji kazi wa utoaji haki.
Amesema uzinduzi rasmi wa wiki hiyo ya sheria katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, itazinduliwa rasmi januari 25 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga katika viwanja vya Zimamoto Manispaa ya Shinyanga na itahimishwa rasmi februari1,2025katika Viwanja vya Mahakama Kuu.

“Kwa kuzingatia maadhimisho ya wiki ya sheria yanafanyika siku za kazi,ambapo wananchi wengi watakuwa kwenye shughuli za utafutaji wa kipato, hivyo utoaji wa elimu kwa mwaka huu umelenga kuwafuata wananchi karibu zaidi na maeneo yao wanayofanyia kazi tofauti na ilivyokuwa hapo awali,”amesema Jaji Mfawidhi Mahimbali.
“Elimu hii ya kisheria tutaitoa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kwa kutumia magari maalumu yatakayokuwa yanahama kutoka eneo moja kwenda jingine,pia tutaongeza wigo wa utoaji elimu kwenye maeneo ya shule za msingi, sekondari na vyuo,”ameongeza.

Amesema ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia watu wengi zaidi, watatumia pia vyombo vya habari kupitia luninga,redio na mitandao ya kijamii.
Amesema katika maadhimisho hayo ya wiki ya sheria pamoja na mambo mengine, elimu hiyo itachagizwa pia na Tamasha kubwa la bonanza la michezo kwa Watumishi wa Mahakama katika ukanda huo.

Pia, amesema katika wiki hiyo ya sheria kauli mbiu itakayokuwa ikijadiliwa kwenye maadhimisho hayo, ambayo inalenga kuelezea nafasi ya Taasisi mbalimbali katika utoaji wa haki, inasema kuwa”Tanzania 2050 nafasi ya Taasisi zinazosimamia haki madai katika kufikia malengo makuu ya dira ya taifa ya maendeleo”.

Amesema kauli mbiu hiyo inawasaidia kutumia mkakati na ufanyaji wa maboresho ya Mahakama hasa wanapoiendea dira mpya ya matumaini ya mafanikio 2050, ya uchumi wa kiwango cha kati ngazi ya juu, na kwamba wao Makahama wamejipanga kufanikisha mpango huo na watakuwa watekelezaji wakubwa wa Dira hiyo ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 hadi 2050.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464