MADIWANI WA KISHAPU WATOA HOJA ZA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU, ELIMU NA AFYA



Na Mapuli Kitina Misalaba

Baadhi ya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wamezungumzia changamoto kubwa zinazowakabili wananchi katika maeneo yao, hususan katika sekta za miundombinu ya barabara, elimu, na afya.

Kauli hizo zimetolewa leo kwenye kikao cha baraza la madiwani cha robo ya pili kilicholenga kujadili taarifa za kata ambapo wamesema kuwa ni muhimu kutengewa bajeti maalum ili changamoto hizo ziweze kutatuliwa kwa uharaka.

Katika kikao hicho, madiwani wamekubaliana juu ya umuhimu wa kushughulikia matatizo yanayohitaji majibu haraka, na pia wameelezea kuridhishwa kwao na juhudi zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali katika kutatua baadhi ya changamoto.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. Francis Philip ameelezea matumaini yake kuwa changamoto zote zilizotolewa na madiwani zitapewa majibu mwishoni mwa robo hii na kuingizwa kwenye bajeti zinazofuata ambapo amewasisitiza wakuu wa idara kuhakikisha wanachukua hatua madhubuti kwa kutekeleza maombi ya madiwani.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Emmanuel Jonhson amekiri kupokea changamoto hizo na kusema kuwa zitaingizwa kwenye bajeti ili kutatuliwa ambapo amesisitiza umuhimu wa maafisa mipango kuhakikisha changamoto hizo zinashughulikiwa kupitia bajeti inayohusika. Madiwani wamekubaliana kwa pamoja kwamba viongozi wa taasisi mbalimbali, kama vile TARURA, RUWASA, na TANESCO, wanapaswa kuhudhuria vikao vya madiwani ili kufikia makubaliano ya pamoja kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.









Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464