Ubovu barabara hospitali ya Mkoa Shinyanga na uhatarishaji maisha ya wagonjwa,kusababisha vifo
Mei 9 mwaka jana pacha wawili ambao ni Kulwa Mahenga na Dotto Mahenga wakazi wa Kijiji cha Lyandu Manispaa ya Shinyanga, wakiwa kwenye pikipiki walipata ajali kwa kugongwa na gari na kufariki dunia papo hapo.
Mapacha Kulwa na Dotto enzi za uhai wao.
Vifo hivyo vilitokea kwenye barabara ya hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kutokana na ubovu wake, tangu kuanza kutolewa huduma katika hospitali hiyo mwaka 2022.
Mama mzazi wa watoto hao Zainab Tagala, anasema kifo cha watoto wake ni pigo kubwa, sababu alikuwa akiwategemea kuendesha familia yake, kutokana na Baba yao kufariki dunia, na kwamba kaka yao mkubwa yeye anajitegemea na familia yake.
“Barabara ya hospitali isingekuwa mbovu,watoto wangu sasa hivi wangekuwa wazima, yani nikifikiria naanza kulia, na siwezi zungumza tena, nenda ukaongee na Kaka yao kwenye mji wake upo jirani tu na hapa, nasikia uchungu sana,”anasema Mama mzazi Zainab.
Kaka wa vijana hao Mohamed Shabani, anasema walipokea taarifa ya ajali ya wadogo zake Kulwa na Dotto kwa mshituko mkubwa, na kwamba waligongwa wakati gari lilipokuwa likikwepa mashimo katika barara hiyo ya hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Shabani anasema,aliwaacha wadogo zake nyumbani kama nguzo ya familia,na baada ya vifo hivyo wamelia na wamenyamaza,, na kuiomba serikali iiangalie barabara hiyo kwa jicho la tatu, sababu inapitiwa na watu wengi na imekuwa ikikatwa na maji pale mvua zinaponyesha.
Kaka wa Marehemu Mohamed Shabani akionyesha kaburi ambalo wadogo zake wamezikwa mara baada ya kupata ajali barabara ya Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga.
Kwa mujibu wa takwimu ambazo zimetolewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John, kwamba kwa siku moja hua wanahudumia wagonjwa zaidi ya 200.
Mwongozo wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga wa mwaka 2014, unaonyesha michoro ya majengo namna itakavyojengwa pamoja na kuwepo na ubora wa barabara.
Sera ya afya ya mwaka 1990 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007 kifungu namba 5 (b) kinazungumzia huduma bora za afya zinazowafikia wananchi wote kwa urahisi.
Muonekano ubovu wa Barabara ya Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga.
Dk.Luzila anasema, hospitali hiyo ilianza rasmi kutoa huduma za matibabu Desemba 29,2022, na kwamba kutokana na uhitaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wa mkoa huo, ilibidi waanze kutoa huduma hivyo hivyo licha ya ubovu huo wa barabara.
Anasema kutokana na ubovu wa barabara hiyo na kutojengwa kwa muda mrefu, amekuwa akilipigia kelele tatizo hilo kwenye vikao mbalimbali vya viongozi, kikiwamo kikao cha kamati cha ushauri cha mkoa huo (RCC) Desemba 15,2023, lakini hakuna utekelezaji wake.
Gari la wagonjwa Ambulance likipita katika barabara mbovu ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Anafafanua ubovu huo wa barabara, umekuwa ukisababisha vifo na kuhatarisha maisha ya wagonjwa, na kwamba magari ya wagonjwa “Ambulance”yamekuwa yakipata ajali huku yakiwa yamebeba wagonjwa, jambo ambalo ni hatari kupoteza maisha.
“Athari za ubovu wa barabara hii ni kubwa, mfano ukiwa umembeba mgonjwa aliyevunjika mifupa au mjamzito, hadi kufika hospitalini hapa atakuwa amepata maumivu makali sana na kuhatarisha afya yake,” anasema Dk.Luzila.
Anasema, pia magari ya hospitali hiyo yamekuwa yakiharibika na kuingia gharama za matengenezo ya mara kwa mara, na kwamba gari moja hadi sasa wamelipaki baada ya kukosa fedha za kulitengeneza.
Dereva wa gari la wagonjwa “Ambulance”katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga John Mabelele, anasema changamoto ambayo wanaipata kutokana na ubovu wa barabara ya hospitali hiyo, ni uharibifu wa magari, ajali, na kwamba wakiwa wamebeba wagonjwa ambao wapo “serious”hua wanalalamika kuumia.
Anasema, pia mvua zinaponyesha barabara ndiyo hua inakuwa mbaya zaidi, sababu mashimo yanafukiwa na maji, na hivyo inakuwa vigumu kuyaona na kujikuta wakivunja “shockup” za magari na kupigiza wagonjwa.
Mgonjwa Letecia Dotto, anasema kipindi anakwenda kupata matibabu kwenye hospitali hiyo, akiwa amebebwa kwenye bajaji, alikuwa akisikia maumivu makali, hasa pale kunapotokea mtikisiko.
Mtumiaji wa barabara hiyo Kuluthumu Mohamed, anasema magari yao yamekuwa yakiharibika mara kwa mara, na haipiti wiki lazima waende kufanya matengezo, na gharama zake si chini ya 200,000.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi, anasema ubovu wa barabara hiyo,imekuwa ikisababisha ajali nyingi, na kuwasihi madereva wa vyombo vya moto, kwamba wanapoitumia wawe makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Anasema ubovu wa barabara siyo ndiyo iwe sababu ya kukithiri kwa ajali, kwamba utii wa sheria za usalama barabarani ni nguzo muhimu ya kuzuia ajali, ikiwamo kuendesha kwa mwendo mdogo ili kukwepa mashimo, na hata chombo hakiwezi kuharibika.
“Siwezi kuchambua kwamba katika barabara hiyo zimetokea ajali ngapi, matukio haya hua tunajumlisha kwa ujumla,na kipindi mwezi mmoja Novemba 2024 tumekamata jumla ya makosa ya barabara 7,920, Magari 5,615 bajaji na pikipiki 2,305, kutokana na kukiuka sheria na kusababisha ajali”anasema Magomi.
Mkuu wa kitengo cha elimu kwa umma kutoka Trafiki Makao Makuu Michael Stephen, anataja takwimu kwamba wameshawafungia madereva 200 lesseni zao, kwa kipindi cha miezi minne, kuanzia Agosti hadi Novemba 2024, kutoka na kukiuka sheria za usalama barabara na kusababisha ajali.
Waziri wa fedha Dk.Mwigulu Nchemba juni 13,2024 akiwa Bungeni Jijini Dodoma akiwasilisha Taarifa ya hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, alitaja takwimu kwamba, jumla ya watu 7,639 wamepoteza maisha kwa ajali za barabarani, kwa kipindi cha miaka mitano 2019-2024 na majeruhi 12,663.
Mratibu wa ujenzi wa miundombinu ya Afya Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu, anasema maeneo yote yakutolea huduma ya Afya, kisera yanapaswa yawe na miundombinu rafiki ya wagonjwa kufika kwa urahisi bila ya kikwazo chochote.
“Kitu ambacho hua tunakizingatia kwenye ujenzi wa huduma za Afya, ni kuhakikisha miundombinu ya usafiri inakuwa rafiki kwa wagonjwa, na kunapotokea changamoto hua tunawasiliana na TARURA kufanya matengezo ya barabara,”anasema Mlyutu.
Meneja Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA)wilaya ya Shinyanga Mhandisi Samson Pamphili, anasema walishapokea maombi ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, na kwamba tatizo ambalo limekwamisha ujenzi wa barabara hiyo linatokana na ufinyu wa bajeti.
Anaeleza kuwa kwa sasa wameshapata fedha kutoka ufadhili wa benki ya dunia sh.bilioni 9 kwa ajili ya kujengwa barabara mbili pamoja na daraja, miundombinu ambayo itasaidia kufika hospitalini hapo kwa urahisi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, anakiri kwamba ubovu wa barabara hiyo ni tatizo kubwa kwa wagonjwa kufika kupata huduma katika hospitali ya mkoa huo.
Anasema, kwa sasa barabara hiyo imeingizwa kwenye mpango wa benki ya dunia, na ujenzi wake unatarajiwa kuanza mwezi Februari au Marchi mwaka huu 2025.
“Barabara hii ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ni mbovu sana, na wananchi wamekuwa wakiipigia kelele, na kipindi cha kiangazi hua kuna vumbi, masika utelezi mkubwa na ina mashimo,lakini serikali ipo katika hatua nzuri ya kuijenga,”anasema Macha.
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi,Ajira na Watu wenye ulemavu, anasema barabara hiyo ilikwama kujengwa sababu ya mifumo ya kifedha, lakini kwa sasa wanasubiri pesa kutoka benki ya dunia ili waanze kuijenga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464