Na Estomine Henry,
SERIKALI wilayani Shinyanga imeendelea kuchukua hatua za
kufuatilia miradi ya maendeleo kwa wananchi lengo kutathimini utekelezaji wa
ilani ya Chama cha Mapinduzi kupitia kazi zinazotekelezwa na Halmashauri.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro alisema hayo Januari,15,2025 katika muendelezo wa ziara ya kutembelea kijiji kwa kijiji nakufanya mikutano ya hadhara kwenye kata za usanda na samuye katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mtatiro akiambatana na wataalam wa Halmashauri, viongozi wa chama
cha Mapinduzi na watendaji ngazi ya kata
na vijiji ili kutoa majibu juu ya kero za wananchi zinazowasumbua muda mrefu.
“Lengo la ziara hii ni kutoa fursa kwa wananchi kueleza changamoto zao ambazo serikali inapaswa kuzitekeleza na sisi
viongozi kuzitolea majibu namna ya utekelezaji wake kupitia miradi”amesema Mtatiro.
AFYA.
Mkuu wa wilaya Mtatiro amemtaka Mtendaji wa kata ya samuye kueleza ukweli juu
ya kiasi cha Shilingi Milion 11.7 za kijiji cha Mwang”halanga zilizokusanywa
kupitia michango ya Shilingi 28,000 kwa
kila kaya zilipokwenda.
Julius Kiyenzi,Mwenyekiti wa kijiji cha Mwang”halanga amesema
kuna kaya 417 kwa mujibu wa sensa ya
watu na makazi ya mwaka 2022 huku akieleza anayetuhumiwa kwa wizi wa shilingi 500,000 ni mkazi mmoja anayetambuliwa kwa jina la Chagu
Tungu.
Mtendaji wa Kata ya Samuye Hellen Kayagila ameeleza shilingi Milioni 11.7 ziko benki ya NMB na hatua iliyomfanya Mtatiro
kupiga simu kwa meneja wa benki na kuthibitisha uwepo wa kiasi hicho cha fedha
na kurudisha matumaini ya furaha kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Edward Maduhu alitoa sababu ya
kukwamishwa na mfumo wa Nest ambao unaruhusu manunuzi
huku Mkuu wa wilaya Mtatiro kuamua kutoa agizo ifikapo januari 27, 2025 zoezi la upauaji jengo
la zahanati ufanyike haraka;
MIUNDO MBINU.
Baadhi ya Wananchi ambao ni Eliasi Mapalala
na Peter Michael wakazi wa kata ya usanda waliiomba
serikali kuwakarabatia miundombinu ya barabara inayotokea usanda
kwenda Manonga.
Mkandarasi wa Wakala wa Barabara mjini na Vijijini (TARURA)
Emmanuel Maige ameeleza barabara ya usanda –Manonga iko katika mpango
wa bajeti ya mwaka 2025/26.
KILIMO.
Wananchi wa kata ya usanda walilamikia juu ya ukosefu wa
mbolea kwa ajili ya kilimo
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri wilaya ya Shinyanga Edward Maduhu
amesema wakala anayesambaza ni mmoja
na vituo vipo vinne
Mkuu wa wilaya Mtatiro ameshauri ni vema kuwe na AMCOS zenye nguvu zitakazosaidia
wakulima kuwa na mbolea za ruzuku na pembejeo .
“Kama hakuna vyama vya msingi imara,tutaendelea kuwa na matatizo ya kudumu ya ukosefu wa mbolea,Mkulima mmoja atakufa peke yake ikiwa hakuna AMCOS” amesema Mtatiro.
UMEME.
Diwani wa kata ya Usanda Forest Nkole amesema huduma ya umeme
iko kwa asilimia 30 kwa kufikia vijiji 3 kati ya 10 na ameiomba serikali kuharakisha
kuwapatia umeme kufikia asilimia 75.
Baadhi ya taasisi za serikali kama shule za kata ya samuye
kama Mwabenda, Manonga hazina huduma ya umeme na walimu wanapata changamoto
katika uendeshaji wa shule.
Mkuu wa wilaya Mtatiro ameeleza serikali imesha saini
mikataba ya usambazaji wa huduma ya umeme kwa kila kitongoji nchini.
ELIMU.
Wananchi Paschal Julius Kasenga mkazi
wa kijiji cha singita alihoji kuhusu michango ya shule inayotolewa na wazazi haitolewi
mrejesho wa shughuli zilizofanyika.
Mtatiro ameagiza wakuu wa shule
kuhakikisha wanatoa taarifa za michango ya shule waliyokubaliana na wazazi ili
kuepusha migogoro.
Mtatiro alisisitiza wananchi kupeleka
watoto shule na hata wakiwa na mapungufu ya vifaa ni vema watote taarifa kwa
wakuu wa shule.
“Usipopeleka
mtoto shuleni utahusika na adhabu ya Shilingi 100,000 au kifungo cha miezi sita
”amesema Mtatiro.
MAJI.
Baadhi ya
wananchi wa kata ya usanda walilamikia juu ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu.
Mtatiro alieleza kuwa mradi wa maji wa Tinde package uko katika hatua ya
manunuzi ya vifaa kwa sasa na muda wowote maji yataanza kuwafikia wananchi.
“Tulifanyia kazi kwa kushirikiana na
katibu wa wizara ya maji, Mbunge wa jimbo solwa na viongozi wa serikali ya India
mkoani Dodoma kujadili na kufikia hatua nzuri na mchakato wa manunuzi ya vifaa unaendelea
kwa sasa”anasema Mtatiro
MADINI.
Wakazi wa
kitongoji cha Mhivi kata ya Usanda Pascal Ntwanga na Maganga Nohiwe walieleza
kuathiriwa na mlipuko ya baruti inayoa athiri watoto
wao na kuharibu nyumba zao kwa nyufa.
Mtatiro ameagiza Ofisi ya madini mkoa wa Shinyanga
kwa kushirikiana na serikali ya kitongoji cha Mhivi kufanya mkutano ili
wananchi watoe changamoto zao na kupanga utaratibu mzuri baina ya wananchi na
mwekezaji.
“Naagiza ofisi ya madini kukutana na
wananchi ndani ya siku 14 kwa kufanya mkutano na wananchi wa kitongoji nakushauri
tujenge nyumba zenye uimara”anasema Mtatiro.
Mwekezaji Abdalah Barageshi akijibu hoja juu ya mlipuko ya mawe inayolalamikiwa na wananchi.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Usanda Edson Jisena akizungumza kwenye mkutano huo.