KATIBU WAZAZI SHINYANGA MJINI AWATAKA WAZAZI KUACHA KUWALAZA CHUMBA KIMOJA WATOTO NA WATU WAZIMA

Katibu wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Shinyanga mjini akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Mwadui baada ya kupanda miti katika maeneo ya ya shule hiyo. 

Suzy Butondo, Shinyanga

Katibu wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Shinyanga mjini  Doris Kibabi amewataka wazazi wote kuepuka kuwachanganya  watoto chumba kimoja na watu wazima, kwani kuna baadhi ya watu wazima ambao ni ndugu lakini hawana maadili mema, ambao wanawaza kuwafanyia ukatili watoto kwa kuwabaka au kuwalawiti.

Hayo ameyasema leo wakati akiwa mgeni rasimi kwenye maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika kata ya Ngokolo katika Shule ya msingi kwa kupanda miti na kuwagawia watoto zawadi mbalimbali zikiwemo pipi na biscuit.

Kibabi amesema baadhi ya watoto wamekuwa wakifanyiwa ukatili na ndugu ambao wanafika kwenye familia kama wageni na wazazi kuwalaza watoto wao pamoja na wageni hao ambao hawajui tabia zao na kuwafanyia ukatili wa kuwabaka na kuwalawiti bila huruma yeyote.

"Tunakeme tabia za watu wanaowafania ukatili watoto, watu hawa wakibainika wachukuliwe hatua kali za kisheria, pia wazazi tuendelee kukaa karibu na watoto wetu ili kuhakikisha wako salama pia wazazi wote tuwalinde watoto hata kama si wa kwako ukimkuta anafanyiwa ukatili chukua hatua usinyamaze " amesema Kibabi.

Aidha amewataka wazazi watoe michango ya chakula mashuleni ili watoto wasishinde njaa kwani wazazi wasipotoa fedha wanawafanyia ukatili kwa kuwashindisha njaa, hivyo hawawezi kufaulu vizuri na hawawezi kushika kile wanachofundishwa.

"Lakini pia tuwaombe walimu wakomeshe tabia za watoto watukutu wanaofundisha watoto wenzao tabia mbaya ikiwa ni pamoja na wazazi kila wanaporudi majumbani wawakague watoto kama wamesoma maana kuna wengine wanaishia njiani ikifika wakati wa kurudi nyumbani na wao wanarudi, lakini ukiwa unamkagua kika siku hawezi kuishia njiani"amesema Kibabi.

Akizungumzia suala la upandaji miti amesema miti imekuwa ikipandwa kila mwaka lakini haionekani kwa sababu ya watu baadhi kujiita miungu mtu kuachilia mifugo yao na kwenda kulisha miti kwa kujiita wenyewe ni viongozi wakubwa hawawezi kukataliwa kuchunga mifugo hiyo.

"Niwaombe hao watu wanaoachia mifugo hiyo waache mara moja tutawachukulia hatua kali za kisheria leo tunapanda miti, tunaomba miti hii isimamiwe ipasavyo ikileta mifugo hiyo muikamate mtuite ili sheria ifuate mkondo wake" amesema Kibabi

Kwa upande wake diwani wa kata ya Ngokolo Victor Mkwizu amesisitiza kuwa miti hiyo inayopandwa iweze kusimamiwa ipasavyo kwani kuna miti iliyopandwa miaka iliyopita haionekani. 






























Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464