Mbunge wa Jimbo la Solwa Mkoani Shinyanga Mh. Ahmed Salum kushoto akikata utepe wakati akikabidhi gari la kubeba wagonjwa (AMBULANCE) katika kituo cha afya tarajiwa Lyabukande katika halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga January 08, 2025.
**
Mbunge wa Jimbo la Solwa Mkoani Shinyanga Mhe. Ahmed Salum amekabidhi gari la Wagonjwa katika Kituo cha afya tarajali cha Lyabukande halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga January 8, 2025 ikiwa ni moja ya mahitaji makubwa kwa wananchi wa kata hiyo.
Akikabidhi gari hilo litakalotumika kusafirisha wagonjwa wakiwemo wajawazito waliokuwa wakipata kadhia na changamoto wakati wa kujifungua kwa kutumia gharama kubwa za kukodi magari binafsi hali ambayo alichangia wengi wao kujifungulia njiani na wengine kupoteza maisha.
Amesema kuwa upatikanaji wa gari hilo ni moja ya maombi aliyowasilisha kwa serikali kupitia Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango alipofanya ziara ya kikazi mkoani Shinyanga, na kwamba moja ya maeneo yenye idadi kubwa ya watu ni Kata za Lyabukande, Mwakitolyo na Didia, Kata ambazo zinahitaji huduma za vituo vya afya na gari za kubeba wagonjwa.
Mh. Ahmed amesema kuwa licha ya eneo hilo kuwa zahanati,lakini limekuwa likitoa huduma zenye hadhi ya kituo cha Afya kutokana na kuhudumia wananchi wa kata zaidi ya tatu pamoja na wakazi kutoka wilaya jirani zinazozunguka eneo hilo.
Aidha amesema kuwa, tayari Serikali imekwisha peleka fedha kiasi cha Shilingi milioni 666.6 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Lyabukande kitakachokuwa kinatoa huduma karibu kwa wananchi waliokuwa wakitumia kati ya laki 2, 3 hadi 5 kukodi magari ya watu binafsi kwenda katika hospitali ya halmashauri,na Rufaa mkoani Shinyanga.
Wakati huo huo amekabidhi pikipiki kwa ajili ya utoaji
wa huduma za chanjo kwa wananchi wa kata hiyo ili watoto wao waweze kupewa chanjo katika mandhari walioko mbali kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za chanjo.
Mganga Mkuu wa halmashauri ya Shinyanga Dkt. Nuru Yunge,amesema kuwa wanayo hospitali moja ya halmashauri, vituo vya afya vitano na zahanati,44 ambazo zinasaidia kutoa huduma kwa wakazi wa halmashauri hiyo ambapo kituo cha afya kimoja na zahanati 5 zinatoka mashirika binafsi.
Dkt. Yunge amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wataarajia kufungua zahanati 7 kutoka katika vijiji vya Nyang’ombe, Songambele, Manyada, Kizungu, Mwamalulu, Mwandutu na Nyida, ikiwa ni mkakakti wa serikali wa kusogeza karibu huduma za afya na wananchi wa maeneo husika.
Aidha, amesema katika fedha zilizotolewa na serikali katika ujenzi wa kituo cha afya Lyabukande jumla ya shughuli 8 zinatarajiwa kufanyika ikiwa ni Pamoja na Jengo la Wagonjwawa Nje,(OPD), Maabara, Jengo la Upasuaji, jengo la kufulia,ukamilishaji wodi ya wazazi,ukamilishaji choo cha nje, mfumo wa maji safi na Mfumo wa umeme vitakavyosaidia kutolewa kwa huduma hiyo
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Shinyanga Ngassa Mboje, amempongeza Mbunge Ahmed Salum kwa kuhakikisha anasimamia suala la upatikanji wa huduma bora za afya kwa wananchi wake,ambapo amekuwa mmoja wa watetezi wa wananchi katika jimbo hilo
Ngassa amewataka wasimamizi wa Gari la kubeba wagonjwa na pikipiki zilizokabidhiwa, kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kutoa huduma kwa wananchi
kwani walikumbana na kadhia kubwa ikiwemo gharama kubwa za kukodi magari kwa watu binafsi
Nao baadhi ya wakazi wa Lyabukande akiwemo Rahel Paulo, Marry Maige na Darusi Bukenda, wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwapatia gari hilo ambalo limekuwa msaada mkubwa kwa jamii hiyo,kwani akina mama wengi walipoteza watoto na wengine kufariki kwa kukosa usafiri wa uhakika na haraka sanjali na kutumia gharama kubwa kukodi magari ya watu binafsi.
Mbunge wa Jimbo la Solwa Mkoani Shinyanga Mh. Ahmed Salum kushoto akikabidhi ufunguo wa gari la kubeba wagonjwa(AMBULANCE) katika kituo cha Afya Lyabukande katika halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga January 08, 2025.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Shinyanga Ngassa Mboje akizungumza kwenye hafla hiyo ya kukabidhi gari la wagonjwa Lyabukande
Mganga Mkuu wa halmashauri ya Shinyanga Dkt.Nuru Yunge akisoma hali utoaji wa huduma za afya katika halmashairi ya Shinyanga kabla ya kukabidhiwa gari la kubeba wagonjwa katika kituo cha Afya Lyabukande