SERENGETI BYTES YATOA ORODHA YA WATANZANIA 100 WALIOCHOCHEA MABADILIKO KATIKA MWAKA 2024

  

Kampuni ya Serengeti Bytes imetangaza rasmi toleo la pili la jarida la Watanzania 100 Wanaochochea Mabadiliko (100 Tanzanian Changemakers 2024), ambalo linahusisha taarifa za watanzania wanaoleta mabadiliko chanya katika sekta mbalimbali nchini.

 Jarida hili linaangazia juhudi za viongozi, wavumbuzi, wabunifu, wajasiriamali, na wanaharakati wanaochangia maendeleo ya kijamii, kiuchumi, na kiteknolojia nchini Tanzania.

Toleo hili la pili linajumuisha wasifu wa watu 100 walioleta mchango mkubwa katika nyanja tofauti. Wakurugenzi wa Serengeti Bytes wanasema jarida hili si tu njia ya kuwaenzi bali pia jukwaa la kuhamasisha Watanzania kuungana katika kujenga taifa lenye ustawi.

“Orodha ya mwaka huu inaonyesha utofauti wa vipaji na kazi za kipekee zinazofanywa na Watanzania kutoka sehemu mbalimbali,” amesema Kennedy Mmari, Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Bytes. “Hawa ni watu wanaoonesha kwa vitendo kuwa mabadiliko yanawezekana kupitia bidii, ubunifu, na kujituma.”

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Serengeti Bytes, Michael Mallya, ameongeza kwa kusema: “Kila aliyeingia katika orodha hii ni ushuhuda wa nguvu ya maono na kushirikiana. Kupitia hadithi zao, tunalenga si tu kusherehekea mafanikio yao bali pia kuhamasisha ushirikiano wa kitaifa katika kuchochea maendeleo.”

Jarida hili limeandaliwa kwa umakini kupitia mchakato ulioshirikisha mapendekezo ya umma, tathmini za wadau, na utafiti wa kina. Kila hadithi inaelezea mchango wa wahusika katika kuboresha maisha ya watu na kujenga jamii zenye ustawi endelevu.

Kwa mujibu wa Serengeti Bytes, mpango huu unalenga zaidi ya kusherehekea mafanikio ya mtu mmoja mmoja, bali pia kuhamasisha mshikamano wa kitaifa. “Jarida hili ni njia mojawapo ya kuleta pamoja fikra na maono ya mabadiliko. Tunataka kila Mtanzania atambue kuwa anaweza kuchangia kujenga taifa lenye nguvu na fursa kwa wote,” ameongeza Mmari.

Orodha hii imegawanywa katika makundi tisa ikigusa sekta mbalimbali ikiwemo Serikali na Uongozi wa Umma, Biashara na Ujasiriamali, Teknolojia na Uvumbuzi, Sekta ya Azaki na Maendeleo, Sekta ya Tafiti na Taaluma, Vyombo vya Habari, Michezo, Sanaa na Burudani, Afya na Ustawi pamoja na Wadau wa Maendeleo wa Kimataifa. 

Katika tolea la mwaka 2024 tumeongeza kipengele cha Wadau/Marafiki wa Maendeleo ya Tanzania kwa lengo la kutambua mchango mkubwa wa watu ambao si raia wa Tanzania lakini wamekuwa na mchango unaostahili kutambuliwa kwa upekee.” ,amehitimisha Mallya. 

Jarida linapatikana kwa njia ya kielektoniki. Kwa maelezo zaidi au kupata nakala yako, tembelea https://changemakers.co.tz/ au wasiliana na Serengeti Bytes kupitia hello@serengetibytes.com.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464