WAFANYABIASHARA NDOGO NDOGO NYAMAGANA JIJINI MWANZA, WAMUOMBOLEZA TIBA LUSHAGARA

 

Viongozi wa Umoja wa Wafanyabiashara ndogo ndogo Nyamagana wakiwasilisha salaam za rambirambi.

                                                       Marehemu Tiba Lushagara

 Na Mutayoba Arbogast

Wafanyabiashara ndogo ndogo katika wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza wameeleza kusikitishwa na kuguswa na kifo cha mfanyabiashara mwenzao, Tiba Lushagara kilichotokea Januari 20 mwaka huu katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwanza, Sekou Toure.

Tiba Lushagara, ametajwa na wafanyabiashara wenzake kuwa alikuwa mtu wa kujitolea kwake kwa nguvu zake zote kudai haki ya kufanyabiashara kwa haki na usawa bila manyanyaso.

Akiwasilisha salaam za rambirambi wakati wa mazishi yake Kijijini kwao Bugombe, Kata ya Kanyigo, Mkoa wa Kagera, Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara ndogondogo Wilaya ya Nyamagana, Matandula Ramadhani, amesema marehemu Tiba Lushagara alikuwa mtu shupavu katika kuongea na kutenda, akisema mojawapo ya mambo ambayo wafanyabiashara hawatamsahau ni pale alipowasilisha maoni na mapendekezo  ya wafanyabiashara kwa mh Rais John Pombe Magufuli mwaka 2019, jambo ambalo lilizaa mazungumzo baina ya viongozi na wafanyabiashara, na angalau kukawepo mazingira nafuu ya ufanyaji biashara.

Naye Zuwena Mahamoud, Katibu wa umoja huo, amesema marehemu Tiba hakuwa mfanyabiashara tu, lakini pia kiongozi  mwenye huruma ambaye alifanya kazi kwa bidii kusaidia wengine, kwani hakuridhika kuona biashara ya mwenzake inatetereka, badala yake angemtia moyo na kumsaidia kwa hali na mali kadri alivyoweza.

"Licha ya misimamo yake mikali katika nasuala aliyoyaamini, hakusita  kurekebisha pale alipogundua hakuwa sahihi kwa kutojua au kupotoshwa, na hivyo kuungana na aliokuwa ametofautiana nao", alisema Zuwena akiongeza kuwa wafanyabiashara waliousindikiza mwili wa marehemu, kilikuwa kielelezo tosha cha umuhimu wake kwa umoja huo.

 Msemaji wa familia, Gregory Ishabakaki ameiombafamilia ndugu na jamaa kuendelea kumsaidia mama yake na marehemu mwenye miaka 83, ambaye alizaa watoto saba, sasa kabaki na mtoto mmoja pekee, huku pia akiwahimiza watoto wawili wa kiume ambao  ni mapacha (26), wasije kumsahau bibi yao.

Ameishukuru Jumuiya ya Wafanyabiashara ndogo wa Nyamagana  kwa majitoleo yao, na wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine hadi kumpumzisha marehemu.

Ni dhahiri marehemu Tiba Lushagara ameacha kumbukumbu itakayoendelea kuhamasisha wengine kupigania usawa katika biashara. Kumbukumbu yake itaishi ndani ya mioyo ya kila mtu ambaye smeguswa, wakiendelea kukumbuka nguvu zake, ujasiri, na umoja aliouunda kati ya wafanyabiashara wadogo. Maisha yake na michango yake itakumbusha kila mtu juu ya umuhimu wa kusimama kwa kila mmoja na kufanya kazi kwa mazingira bora ya biashara kwa wote.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464