Wanawake wa UWT Mkoa wa Shinyanga wametoa tamko la kuunga mkono kampeni ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vitendo na kutoa tamko la kumpongeza kwa kuteuliwa na Halmashauri kuu ya CCM kuwa mgombea pekee wa kiti cha Urais kupitia Chama cha Mapinduzi.
Baada ya tamko hilo lililotolewa kwa niaba ya Mwenyekiti na katibu wa UWT Mkoa wa Shinyanga, Wanawake hao wameonyesha mfano wa kutumia nishati safi ya kupikia aina ya gesi tukio lililotanguliwa na upandaji wa miti katika eneo la ujenzi wa nyumba ya Mwenyekiti wa Jumuia hiyo katika viwanja vya Mwalugoye lengo likiwa ni kurejesha uoto wa asili ulioharibika baada ya miti kukatwa, na hivyo kuchangia kupunguza mabadiliko ya tabianchi.
Na Mwandishi wetu kutoka Shinyanga.
Nao baadhi ya wanawake wa UWT Mkoa wa Shinyanga waliohudhuria hafla hiyo akiwemo christina Gule ambaye ni Mbaraza na Tatu Shabani ambaye ni Mwanachama wamesema matumizi ya nishati safi ya kupikia aina ya gesi na umeme yametokomeza mauaji ya wanawake waliokuwa wanatuhumiwa kuwa ni wachawi kutokana na kuwa na macho mekundu kwa kusababishwa na matumizi ya nishati chafu ya kuni, mkaa na kinyesi cha ng'ombe.
Awali akisoma tamko hilo, Katibu wa UWT Mkoa wa Shinyanga, Bi. Habiba Ismail Msim, amesema wanawake wa UWT wameamua kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa mambo matatu, la kwanza kuunga mkono agenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, pili ni kumpongeza kwa kuteuliea halmashauri kuu ya CCM kuwa mgombea pekee wa kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu ujao na tatu kumpongeza kwa kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake CCM Mkoa wa Shinyanga, Bi. Grace Samwel, amewataka wanawake wa UWT, baada ya Mkutano Mkuu wa CCM kumalizika, kuvunja makundi yao na kufanya kazi kama timu hali ambayo itadumisha uzalendo, weledi na ustahimilivu ndani ya chama cha Mapinduzi.