WAZIRI AHIMIZA WANAJAMII KURIPOTI VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WATOTO KWA HARAKA SIMU NAMBA 116

 

WAZIRI AHIMIZA WANAJAMII KURIPOTI VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WATOTO KWA HARAKA SIMU NAMBA 116

                                     Picha: Waziri wa Maendeleo  ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima.

                                          Na Mutayoba Arbogast, Bukoba

Imebainika kuwa sababu mojawapo ya kuendelea kufanyika kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hasa wale wenye umri mdogo kabisa, ni kwa sababu baadhi ya   wazazi, walezi na jamii hawajui wapi waweze kupata msaada wa haraka katika kuripoti vitendo hivyo.

Bibi Anastazi Kashemeile (si jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 70, mkazi wa kijiji kimojawapo wilayani Missenyi mkoani Kagera, anayeishi na mjukuu wake wa kike anayesoma darasa la nne, ambaye wazazi wake ni marehemu, anamuangalia mjukuu wake kana kwamba kuna kitu hakiko sawa.Jicho lake linamuangalia toka utosi hadi unyayo.

Naam, anagundua kuna jambo si bure. Kwa sauti ya upole anamkalisha chini mjukuu wake na kumuuliza kulikoni tangu jana anamuona akitembea kwa kuchechemea, aliteguka, alichomwa na mwiba?.

Kwa dakika kadhaa mtoto hasemi chochote bali akibubujikwa na machozi.Bibi kwa ustadi mkubwa anamtuliza na kuendelea kumuongoza na kumvuta kwenye mazungumzo.

"Mzee Makwito (si jina lake halisi), juzi alinivuta chumbani, akanifanyia kitu kibaya".

Bibi anaingiwa mchecheto na simanzi, anamuona mzee huyo ambaye ni jirani yake ibilisi mkubwa, hajui afanyeje kumkabili. Anamkimbilia jamaa yake kuomba msaada wa mawazo, ila anamshauri waachane na hilo jambo, maana litawachukulia muda na gharama kufuatilia suala hilo mahali ambapo wangetoa taarifa: lakini hata wasijue ni wapi, kwa balozi wa nyumba kumi, shuleni, polisi au...Wanakubaliana kuachana nalo, huku mtoto akiendelea kuugulia maumivu kimyakimya, akikandwa na kunyweshwa dawa za miti shamba.

Huyu bibi ni kiwakilishi cha wengi ambao hushindwa kuripoti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Dk Dorothy Gwajima,Waziri wa Maendeleo  ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, akiandika mwezi Desemba 2024 katika Ukurasa wake wa X ( zamani Twitter), anawahimiza jamii pana  kuyamulika matendo ya ukatili kwa watoto, kuyaibua na kutoa taarifa mapema mahali sahihi ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati kabla madhara hayajatokea.

Nawaasa Wazazi na Walezi kuachana na tabia ya kuwaacha Watoto peke yao na kuwafungia ndani na wao kwenda kwenye shughuli zao ikiwemo starehe pasipo uangalizi na ulinzi makini wa watoto ..." ameandika Dk Gwajima.

Dk Gwajima atoa namba za simu huduma ya haraka

Aidha katika kuhakikisha habari za ukatili au viashiria vyake dhidi ya watoto, vinapata msukumo kutoka wizara yake, wananchi watume taarifa kwanjia simu kwa kupiga au kuandika ujumbe kwenda namba ( huduma ya bure) 116 inayopatikana saa 24 kila siku, au Kituo cha Wizara kwa namba  0766400168/0734986503/0262160250/0769608130 na WhatsApp 0744112233 au kukata rufaa kwake kwa namba 0765345777.

Dk Gwajima, katika kuonesha umuhimu wa matumizi ya mitandao kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa watoto, anasema akimnukuu raia mwema "Tarehe 28 Desemba, 2024 asubuhi nilipokea ujumbe kwa njia ya simu (sms) kutoka kwa Raia Mwema anayeishi Mkoa wa Tabora, Igunga, nanukuu “kuna binti ana mtoto ila lengo lake ni kama anataka kumuua kwa sababu imekuwa ni tabia yake kumfungia ndani na kuondoka kwenda anakoenda na kurudi siku nyingine. Hivo tunaomba msaada wenu tafadhali".

Anasema aliwasiliana na uongozi wa mkoa Tabora ambao nao waliwasiliana na uongozi wa Wilaya ya Igunga ambao, mara moja walituma Maafisa wa Dawati la Jinsia wakiwemo Ustawi wa Jamii kwenda kufanya ufuatiliaji, na kumkuta  mtoto ( umri miaka miwili) akiwa na viashiria vyenye hatari kwa usalama wa mtoto ikiwemo malezi , makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.

Iligundulika kuwa mama huyo alikuwa mraibu wa pombe, akiwa anamfungia mtoto nyumbani na yeye kwenda kunywa pombe usiku kucha, na pia kukiwa na mgogoro wa ndoa, mambo yaliyolazimu mtoto huyo kukabidhiwa kwa ndugu wa mama yake, huku hatua nyingine zaidi zikiendelea kuchukuliwa  ikiwemo kumsaidia mama huyo kisaikolojia kuondokana na pombe.

Kwa kujua umuhimu wa mitandao kufikisha habari kwa haraka, na umuhimu wa matumizi ya namba ya simu 116, Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) iliwahi kuendesha Kipindi  mubashara cha  Redio  kilichorushwa Juni 2024 kupitia Radio Shnuz FM iliyoko manispaa ya Bukoba ambapo wananchi  walielimishwa kuhusu kutoa taarifa za vitendo vya ukatili huku, wasikilizaji wakipata fursa ya kutoa maoni yao.

Waziri Dk Gwajima anazidi kuzikumbusha Kamati za ulinzi wa watoto kila Wilaya/ Halmashauri kuanzia ngazi ya Mtaa, Kijiji na Kata, kusimama imara zaidi kwenye nafasi zao katika kusimamia ba kuelimisha na kuhamasisha jamii, kupokea taarifa na kuchukua hatua stahiki.

Waziri huyo anaelekeza zaidi akisema,"Mwananajamii ukipata taarifa za usalama mdogo wa mtoto/watoto, timiza wajibu wako wa kutoa taarifa kwa Dawati la jinsia la watoto au kwa Afisa ustawi wa jamii".

Watoto wamekuwa ni waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili kwa kuwa hawana uwezo wa kujilinda au kujitetea wenyewe, kama mtoto wa miaka 06 Grayson Kanyenye aliuawa tarehe 25 Desemba 2024 huko Dodoma.

Kwa upande wa mkoa wa Kagera Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa  tangu Januari hadi Desemba 2024, watuhumiwa 14 wa kesi zilizohusisha watoto na wanafunzi walipatiwa adhabu mbalimbali, zikiwemo kulipa faini, kuchapwa viboko, au kifungo cha nje na kuwa kesi nne ziliishia kwa watuhumiwa kuhukumiwa vifungo vya muda tofauti kulingana na makosa yao.

Changamoto katika kuripoti matukio ya ukatili kwa watoto

Licha ya juhudi kubwa za serikali kupambana na vitendo vya ukatili, kuna changamoto kadhaa katika kufikia malengo kutokana na baadhi ya watoa huduma au wenye mamlaka kuwa na mwitikio mdogo au kutojali, mfano mwandishi amejaribu kupiga simu namba 0262160250 na akajibiwa kuwa simu hiyo haiwezi kupita kwani haijalipiwa!!

Mwezi Oktoba mwaka 2022 Mwandishi wa habari hii aliripoti tukio la ukatili kwa simu kupitia namba 116, mtoto kubakwa wilayani Missenyi, na kila alipofuatilia kujua hatua walizochukua, kulikuwa na mwitikio hafifu.

Hata Afisa mmoja wa ulinzi  na usalama ngazi ya mkoa (jina na cheo chake vinahifadhiwa) alipewa taarifa na kuahidi kulishughulikia baadaye kwa kuwa alikuwa katika pilikapilika za siku ya kuhitimisha mbio za mwenge mkoani Kagera, na hata alipopigiwa tena siku tatu baada ya shughuli hiyo, alimuuliza mwandishi"Hivi una maslahi gani na suala hilo?".

Hata hivyo kutokana na juhudi mbalimbali za wadau wa maendeleo ya watoto, tarehe 15 Machi 2023, Mahakama ya wilaya ya Missenyi ilimtia hatiani mshakiwa huyo kwa kifungo cha miaka 30 jela.


P

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464