WAZIRI MKUMBO-ATAKA WAWEKEZAJI WAZAWA KUANAGALIWA KWA JICHO LA PEKEE

Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited David Mulokozi aliyevaa suti  akisalimiana na waziri wa Nchi ofisi ya Rais Mipango na uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo leo alipotembelea kiwanda hicho.PICHA: JALIWASON JASSON 
 Na Jaliwason Jasson, MANYARA

WAZIRI wa Nchi ofisi ya Rais Mipango na  uwekezaji  Prof. Kitila Mkumbo amekiagiza Kituo cha uwekezaji Tanzania(TIC) kuwaangalia wawekezaji wazawa kwa jicho la pekee huku Shirika la viwango Tanzania(TBS) na Tume ya ushindani nchini(FCC) akiwaagiza kudhibiti bidhaa feki zinazozalishwa mitaani na kudumaza wawekezaji wazawa.

 Mkumbo ametoa agizo hilo leo Mjini Babati mara baada ya kutembelea kiwanda cha Mati Super Brands Limited kinachomilikiwa na mwekezaji mzawa David Mulokozi.

"TIC wawekezaji kama hawa muwape jicho la pekee kila wanachohitaji wapewe ili waweze kufanya uwekezaji wao,"amesema Mkumbo

Prof. Mkumbo amesema uwekezaji unaofanywa unasaidiwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika kutoka Bwawa la Julius Nyerere pamoja na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mjini Babati ( BAWASA) ambao ndio wanatoa huduma ya maji kwa mwekezaji huyo.

Aidha amesema suala la bidhaa feki lililoelezwa na Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited David Mulokozi  amesema wanalichukua kwa uzito mkubwa.

Prof. Mkumbo amesema TBS na FCC wahakikishe wanadhibiti bidhaa bandia ambazo kuwepo kwa bidhaa bandia zinaathiri uchumi na upatikanaji wa Kodi.

Amesema licha ya ubunifu anaofanya mwekezaji huyo wa kuboresha mifumo  amesema ajitahidi kuhakikisha vijana wanapata ajira ili kusaidia serikali.

Amesema kuhusu hoja ya  Mulokozi ya  mabadiliko ya sheria kuwa na athari kibiashara kuanzia Februari mwaka huu  wataanzisha chombo cha kusimamia masuala yote ya uwekezaji na sheria itabadilika.

"Mabadiliko ya mara kwa mara ya sera na sheria tunazifanyia kazi  na serikali itaendelea kumuunga mkono mwekezaji ili afanikiwe,"amesema 

 Naye Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited akitoa taarifa yake amesema ulipaji wa Kodi umekuwa ukiongezeka kila mwaka ambapo mwaka 2022 walilipa sh. Bil. 7.7, mwaka 2023 Bil.7.9 na mwaka 2024 wamelipa Kodi sh. Bil. 8.

Mulokozi amesema wana wafanyakazi 269 ambapo wakudumu ni 147 na wa  kawaida ni 122.

Mkurugenzi huyo amesema changamoto waliyo nayo ni kukosa chupa kutoka kiwanda cha Kioo Limited na kulazimika kuagiza chupa kutoka Kenya au Omani.

 Ameitaja changamoto nyingine ni uwepo wa bidhaa bandia, mabadiliko ya sera na sheria ya Kodi ambayo inawalazimu kulipa kodi kabla ya uzalishaji.


      MWISHO.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464